Sensa ya Uzalishaji Viwandani ya mwaka 2013 imehusisha viwanda vyote vyenye maeneo ya kudumu Tanzania Bara kwa mujibu wa Viwango vya Kimataifa vya Mgawanyo wa Shughuli za Uzalishaji na Utoaji Huduma (ISIC) toleo Namba 4 ili kuhakikisha ulinganishi kimataifa. Sensa hii imejumuisha viwanda vyote vilivyojishughulisha na Uchimbaji madini na mawe; Utengenezaji wa Bidhaa Viwandani; Uzalishaji na usambazaji wa Umeme, gesi, mvuke na kubadilisha hali (joto/baridi); na Kukusanya, kutibu na kusambaza maji. Hata hivyo, sekta ndogo ya utengenezaji wa bidhaa viwandani ndiyo inayoongoza katika sekta zote ndogo za uzalishaji viwandani. Kwa hiyo, mwelekeo wa ukuaji wa sekta nzima ya viwanda kwa kiasi kikubwa, ulitegemea uzalishaji wa sekta hii ndogo.

Utengenezaji wa bidhaa viwandani unahusu ubadilishaji wa malighafi kuwa bidhaa mpya kwa kubadilisha muundo na maumbo. Bidhaa zinazobadilishwa ni malighafi ambazo zinatokana na kilimo, misitu, uvuvi, uchimbaji madini na mawe pamoja na bidhaa za shughuli nyingine za utengenezaji wa bidhaa viwandani ambazo ni malighafi kwa sekta hii. Shughuli za ubadilishaji, urekebishaji wa bidhaa pia hutambulika kama utengenezaji wa bidhaa viwandani.

Madhumuni ya ripoti hii ni kuwasilisha kwa muhtasari, matokeo muhimu yanayohusu Sensa ya Uzalishaji Viwandani ili kutoa rejea muhimu juu ya nini kinapatikana kwenye ripoti kuu. Ripoti imetoa kwa ufupi, matokeo muhimu yanayohusu aina na mifumo mbalimbali ya viwanda husika, ajira na malipo yake, pato ghafi, gharama za uzalishaji na ongezeko la thamani. Matokeo haya yamegawanyika kulingana na aina ya uzalishaji, ukubwa wa kiwanda kulingana na idadi ya wafanyakazi, eneo la kijiografia mahali kiwanda kilipo na hali ya umiliki.

Bonyeza HAPA kupata Muhtasari wa ripoti ya Sensa ya Uzalishaji Viwandani 2013