WANANCHI WAHIMIZWA KUTOA TAARIFA SAHIHI WAKATI WA KUTOA TAARIFA KATIKA UTAFITI WA MAPATO NA MATUMIZI YA KAYA BINAFSI TANZANIA BARA WA MWAKA 2017/18

Wananchi wamehimizwa kutoa taarifa sahihi kwa wadadisi wa Utafiti wa Mpato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18 unaoendelea kufanyika nchini.

Wito huo umetolewa na wakuu wa mikoa ya Geita, Kagera, Mwanza, Mara na Shinyanga wakati wa uhamasishaji wa utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18 katika mikoa yao.

Kwa pamoja viongozi hao wametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilikifu katika kufanikisha zoezi hili linaloendelea kufanyika nchini kwa kipindi cha miezi kumi na mbili na linatarijiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.

“Nawasihi wananchi wote kwa kaya zile ambazo zimechaguliwa kushiriki katika utafiti huu kuwapokea na kuwapa ushirikiano wa kutosha wadadisi. Toeni taarifa sahihi na za uhalisia kuhusu mapato na matumizi yenu ili Serikali iweze kupata Takwimu za hali halisi ya maisha ya mtanzania,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali (Mst) Salum M. Kijuu

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab R. Telack amewatoa hofu wananchi kuwa wasihofie kutoa taarifa kwani wadadisi wamepitia katika mafunzo maalum pamoja na kula kiapo cha kutunza siri hivyo taarifa watakazozitoa zitatumika kwa ajili ya masuala ya kitakwimu pekee.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima amewataka wananchi kutohofia kuhusu utafiti huu kwani hautasimamisha shughuli zao za kila siku bali mdadisi pindi atakapofika kwenye kaya watakubaliana muda wa kufanya mahojiano mara baada ya mwanakaya kumaliza shughuli zake za kiuchumi.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Injinia Robert Gabriel amesema utafiti huu ni muhimu kwa maendeleo ya taifa kwasababu utatoa takwimu za hali ya umaskini na takwimu nyingine ili kusaidia Serikali na wadau wengine kutathmini hatua zilizofikiwa katika kutimiza malengo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yakiwemo yale yaliyoanishwa katika Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) na Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals – 2030-SDGs).

Utafiti huu unaoendelea nchini unatarjiwa kukusanya taarifa kutoka katika kaya binafsi zinazohusu Kaya na Wanakaya, Uzazi na Unyonyeshaji, Elimu, Afya, Uraia, Uhamiaji, Ulemavu, Bima, Hali ya Ajira, Biashara na Mapato ya Kaya na Makazi ya Kaya.

Taarifa zingine zitakazokusanywa ni pamoja na matumizi ya Nishati, Huduma za Maji Safi na Maji Taka, Utalii wa Ndani, Uwekezaji wa Kaya, Matumizi ya Kaya ya Huduma za Kifedha, Upatikanaji wa Usalama wa Chakula, Matumizi, Mazingira, Umiliki wa Vitambulisho Mbalimbali, Kilimo na Mifugo, Matumizi ya Muda kwa kila Mwanakaya Mwenye Umri wa Miaka 5 au zaidi, Mapato na Matumizi ya kila Kaya na Mwanakaya mwenye Umri wa Miaka 5 au zaidi pamoja na taarifa za umiliki wa mali kwa jinsia.

…Mwisho…