PATO LA TAIFA ROBO YA TATU

(JULAI – SEPTEMBA) YA MWAKA 2015

 

Takwimu za Pato la Taifa katika kipindi cha Julai – Septemba mwaka 2015 zinaonesha kuwa, uchumi ulikua kwa kasi ya asilimia 6.3 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 5.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2014, kama inavyoonekana kwenye mchoro namba 1.

 Mchoro Na. 1: Kasi ya Ukuaji wa Pato la Taifa kwa Robo ya Tatu, Julai - Septemba, 2006 – 2015

Shughuli za kiuchumi ambazo zilikua kwa kasi kubwa ni pamoja na Ujenzi (asilimia 17.6), Uchukuzi na Uhifadhi (asilimia10.6), Uendeshaji Serikali na Ulinzi (asilimia 10.6) na Uchimbaji Madini na Kokoto (asilimia 8.0). Aidha, katika kipindi cha Julai – Septemba 2015, shughuli za kiuchumi za Kilimo, Uzalishaji Viwandani, Umeme, Biashara za Jumla na Rejareja, Habari na Mawasiliano, Fedha na Bima zilikua kwa kasi ndogo ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2014.

Katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2015, viashiria vingi vya kiuchumi vimeonesha kutengemaa/kutoyumba ambapo thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi iliongezeka kwa asilimia 3.3. Bidhaa na huduma zilizochangia ongezeko hili ni pamoja na dhahabu, almasi, madini mengine na utalii. Thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa kutoka nje zilipungua kwa asilimia 0.58, ambapo malighafi na bidhaa za walaji zilizoagizwa kutoka nje ya nchi katika kipindi cha Julai – Septemba, 2015 zilipungua ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2014.

Tathmini ya ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2015 inaonesha kuwa, jumla ya thamani ya Pato la Taifa ni Shilingi trilioni 71.7 kwa bei za miaka husika ikilinganishwa na Shilingi trilioni 60.4 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka 2014. Vilevile, jumla ya thamani ya Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2007 katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2015 ni Shilingi Trilioni 33.1 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 30.9 zilizopatikana katika kipindi kama hicho mwaka 2014 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 6.9.

Maoteo ya Pato la Taifa kwa mwaka 2015 yanayotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango yanakadiriwa kuwa Shilingi trilioni 89.1 kwa bei za mwaka husika na Shilingi trilioni 44.1 kwa bei za mwaka 2007. Kutokana na takwimu za Pato la Taifa kwa kipindi cha Januari hadi Septemba, kama hakutakuwa na misukosuko ya kiuchumi duniani inategemewa kuwa maoteo tarajiwa yatafikiwa.

Bonyeza hapa kupata Taarifa zaidi ...