MAELEZO YALIYOTOLEWA NA MKURUNGEZI MKUU OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU WAKATI WA KUZINDUA MATOKEO YA MAREJEO YA FAHIRISI ZA BEI ZA TAIFA KUTOKA 2007 HADI 2011/12, TAREHE 08 FEBRUARI, 2016

Utangulizi

Ndugu Waandishi wa Habari, napenda kutumia fursa hii kuwakaribisha kwa mara nyingine tena katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kuwashukuru kwa kuitikia mwito wa kuhudhuria mkutano huu. Naomba niwakumbushe kwamba, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndiyo yenye mamlaka ya kuratibu ukusanyaji, uchambuzi na utoaji wa takwimu rasmi nchini kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

Lengo kuu la mkutano huu ni kuwafahamisha kuhusu marejeo ya Fahirisi za Bei za Taifa kutoka mwaka 2007 hadi 2011/12 yaliyofanyika kwa kutumia matokeo ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa mwaka, 2011/12. Nitazungumzia kwa kifupi mambo yafuatayo:-

 1. .Fahirisi za Bei za Taifa zilizokuwa zinatumika hadi Desemba, 2015,
 2. .Mchanganuo mpya wa bidhaa na huduma za jamii zinazotumiwa na kaya kwa mwaka 2011/12 ukilinganisha na mwaka 2007 na
 3. .Mizania mpya ya matumizi ya kaya kwenye bidhaa na huduma mbalimbali baada ya kufanya marejeo,

Ndugu Waandishi wa Habari, Fahirisi za Bei za Taifa ni kipimo cha kitaalamu ambacho hutumika kukokotoa kiwango cha Mfumuko wa Bei kwa vipindi viwili tofauti. Fahirisi za Bei zimeendelea kuwa ni kiashiria muhimu cha kiuchumi katika kupima mwenendo wa bei za bidhaa na huduma za jamii (Mfumuko wa Bei) na hutumika kama kigezo kimojawapo cha kupima hali ya maisha ya wananchi. Matumizi mengine makubwa ya Fahirisi za Bei ni pamoja na;

 1. .Kupima na kuboresha sera za kifedha na mipango ya kiuchumi ya kuthibiti mfumuko wa bei,
 2. .Ni kigezo kimojawapo kwenye kukadiria Pato la Taifa ,
 3. .Husaidia kupima uwezo wa fedha katika manunuzi ya bidhaa na huduma za jamii katika vipindi tofauti na
 4. .Hutumika kuboresha mishahara ya wafanyakazi na mafao ya wafanyakazi waliostaafu.

 

 

Maelezo kwa Kifupi Kuhusu Fahirisi za Bei za Taifa Zilizokuwa Zinatumika hadi Mwezi Desemba, 2015

Ndugu Waandishi wa Habari, Fahirisi za Bei za Taifa zilizokuwa zinatumika hadi mwezi Desemba, 2015 zilikuwa zinakokotolewa kwa kutumia bei za bidhaa na huduma zipatazo 224 zikiwa ni pamoja na bidhaa 70 za vyakula na 154 zisizo za vyakula. Bei hizo zilikuwa zinakusanywa kutoka mikoa 21 ya Tanzania Bara. Bei za mwezi Septemba, 2010 zilikuwa zinatumika kama bei za mwezi wa kizio.

Ndugu Waandishi wa Habari, kati ya vigezo muhimu vinavyotumika kupata Fahirisi za Bei zinazoonyesha uhalisia wa matumizi ya kaya binafsi ni pamoja na mizania. Mizania ni kiwango cha matumizi ya kaya kwenye bidhaa au huduma kwa kipindi cha mwaka mmoja. Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa mwaka 2007 uliofanyika katika maeneo ya mijini na vijijini ulionyesha kuwa, matumizi makubwa ya kaya yalikuwa kwenye bidhaa za vyakula zikiwa na asilimia 47.8 ya matumizi yote yakifuatiwa na usafiri asilimia 9.5. Matumizi madogo zaidi yalikuwa kwenye huduma za afya kwa asilimia 0.9.

Lengo la Kufanya Marejeo ya Fahirisi za Bei za Taifa

Ndugu Waandishi wa Habari, lengo kuu la kufanya marejeo ya Fahirisi za Bei za Taifa kutoka mwaka 2007 hadi 2011/12 ni kukokotoa upya orodha ya bidhaa na huduma wakilishi za walaji zinazoonyesha hali halisi ya matumisi ya kaya kutokana na matokeo ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa mwaka 2011/12.

Kwa kawaida, bidhaa na huduma za jamii zinazotumika kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa hubadilika kulingana na wakati, mitindo, kipato, aina ya bidhaa na mwelekeo wa matumizi ya kaya. Mabadiliko hayo husababisha bidhaa na huduma zinazotumika kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa kupitwa na wakati na kutoa vigezo vya kiuchumi ambavyo havionyeshi hali halisi. Kulingana na taratibu za Kimataifa, marejeo ya Fahirisi za Bei yanatakiwa yafanyike angalau kila baada ya mwaka mmoja lakini kwa nchi zinazoendelea inashauriwa kufanyika kila baada ya miaka mitano. Kwa mara ya mwisho hapa Tanzania, marejeo ya Fahirisi za Bei za Taifa yalifanyika mwaka 2007.

Ndugu Waandishi wa Habari, malengo mengine ya kufanya marejeo haya ni pamoja na;

 1. .Kukokotoa mizania mipya zitakazotumika kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa,
 2. .Kuboresha orodha ya maeneo ambayo mara nyingi jamii hununua bidhaa au hupata huduma mbalimbali,
 3. .Kuboresha mbinu na kanuni zinazotumika kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa,
 4. .Kuboresha mfumo wa kompyuta unaotumika kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa na
 5. .Kupanua wigo wa kukusanya bei kwa kujumuisha mikoa minne mipya iliyoanzishwa kati ya mwaka 2007 na 2011/12

Marejeo haya yamesaidia kuboresha mbinu na kanuni zinazotumika kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa ambazo ni kigezo muhimu katika kupima mwenendo halisi wa bei na uwezo wa fedha katika manunuzi ya bidhaa na huduma kwa vipindi tofauti.

Matokeo ya Marejeo ya Fahirisi za Bei za Taifa kutoka Mwaka 2007 hadi Mwaka 2011/12

Ndugu Waandishi wa Habari, naomba ifahamike kuwa, mbinu na kanuni zilizotumika wakati wa kufanya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa mwaka 2011/12 ziliboreshwa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na Utafiti kama huo uliofanyika mwaka 2007. Kwa kuwa Tafiti hizi mbili zilitumia mbinu na kanuni tofauti, mchanganuo wa matumizi ya kaya kwa mwaka 2011/12 hauwezi kulinganishwa moja kwa moja na mchanganuo uliotokana na Utafiti wa mwaka 2007. Hata hivyo, matokeo ya mwaka 2011/12 yatasaidia kuonyesha picha ya mwenendo wa mchanganuo wa matumizi ya kaya kutoka mwaka 2007 hadi 2011/12.

Ndugu Waandishi wa Habari, matokeo yanaonyesha kuwa, mizania ya matumizi ya kaya kwenye bidhaa za vyakula imepungua hadi asilimia 38.5 mwaka 2011/12 kutoka asilimia 47.8 mwaka 2007. Mwenendo huu unaashiria kupungua kwa umaskini wa kipato kwenye kaya kwa kuelekeza matumizi mengine kwenye bidhaa zisizo za vyakula kama usafiri, mawasiliano, makazi, maji na nishati. Ikumbukwe kwamba, pamoja na kwamba mizania ya matumizi ya kaya kwenye bidhaa za vyakula imepungua lakini bado bidhaa za vyakula ndizo zinaongoza kwa kuwa na mizania mikubwa ya matumizi ya kaya kwa mwaka.

Ndugu Waandishi wa Habari, makundi mengine yalioonyesha kuwa na mizania mikubwa ya matumizi ya kaya mwaka 2011/12 ni pamoja na Usafiri asilimia 12.5 kutoka asilimia 9.5 mwaka 2007, Makazi, Maji na Nishati asilimia 11.6 kutoka asilimia 9.2 mwaka 2007 na Mavazi na Viatu asilimia 8.3 kutoka asilimia 6.7 mwaka 2007. Aidha, kumekuwa na ongezeko la zaidi ya mara mbili ya matumizi ya kaya kwenye kundi la Mawasiliano asilimia 5.6 ikilinganishwa na asilimia 2.1 ilivyokuwa mwaka 2007. Makundi mengine yaliyobaki hayakuwa na mabadiliko makubwa kutoka mwaka 2007 hadi 2011/12 na kiwango cha matumizi ya kaya kilikuwa chini ya asilimia 7.0 ya matumizi yote ya kaya kwa mwaka.

Ndugu Waandishi wa Habari, marejeo haya yameongeza wigo wa bidhaa na huduma zinazotumika kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa hadi kufikia 278 zikiwa ni pamoja na bidhaa 97 za Vyakula na Vinywaji Baridi na bidhaa 181 zisizo za vyakula. Kuna ongezeko la bidhaa 54 muhimu zinazotumiwa na kaya baada ya kufanya marejeo. Aina za bidhaa zinazotumika kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa zimeongezeka hadi 336 kutoka 262 zilivyokuwa mwaka 2007. Hii inamaanisha kuwa kuna ongezeko la aina mbali mbali za bidhaa sokoni ambazo zinampa mlaji wigo mpana zaidi wa kuchagua bidhaa anayohitaji kulingana na wakati na kipato chake.

 

Hitimisho

Ndugu Waandishi wa Habari, kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza kwenye mchanganuo wa matumizi ya kaya kwa mwaka 2011/12 ikilinganishwa na mwaka 2007, mwenendo wa bei za bidhaa na huduma nao utabadilika kulingana na mizania mpya. Hata hivyo, hakutakuwa na mabadiliko ya takwimu za Mfumuko wa Bei wa Taifa ambao ulikokotolewa kabla ya kufanya marejeo haya. Hii ni kwa sababu utaalamu uliotumika kufanya marejeo haya ulizingatia mbinu na kanuni zinazopendekezwa Kimataifa kama Shirika la Kazi Duniani (ILO), Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Shirikisho la Afrika Mashariki (EAC) na Shirikisho la Maendeleo la Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).