Mabadiliko ya Kipindi cha Kizio cha Mizania kutoka mwaka 2011/12 hadi 2017/18 na Kipindi cha Kizio cha Bei kutoka Mwezi Desemba 2015 hadi Desemba, 2020

 

  1. Utangulizi

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni taasisi inayotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, sura namba 351. Majukumu ya NBS ni pamoja na utoaji, uratibu na usimamiaji wa upatikanaji wa takwimu rasmi nchini. Fahirisi za Bei za Taifa (FBT) ni moja ya takwimu zinazozalishwa na NBS kwa kila mwezi. FBT ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma za jamii zinazotumiwa na kaya binafsi nchini. FBT ni kiashiria cha kimkakati kinachotumika katika uratibu wa uchumi mpana, hususan katika mienendo yake pamoja na athari zake kwenye uchumi.

 

  1. Miongozo ya Kimataifa

Miongozo ya kimataifa inayoratibu ukokotoaji wa bei inasisitiza kufanya marejeo ya Fahirisi za Bei angalau mara moja katika kipindi cha miaka mitano. Miongozo hii huandaliwa kwa pamoja na wataalamu kutoka nchi mbalimbali wakilishi wa nchi zilizoendelea na zinazoendelea na huidhinishwa na Kamisheni ya Kimataifa ya Takwimu (UNSC). Wadau wakuu wa kufuatilia utekelezaji wake ni shirika la Fedha Duniani (IMF) na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Ili kuendana na miongozo hii, Tanzania kama nchi nyingine inafanya marejeo ya FBT kila baada ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi. Marejeo yanayofanyika kwa sasa yatahuisha mizania zinazotumika kukokotoa FBT kutoka mwaka 2011/12 hadi 2017/18. Aidha, kizio cha bei nacho kitabadilika kutoka mwezi Desemba 2015 hadi Desemba, 2020. Matumizi ya kizio cha bei cha mwezi Desemba kilikubalika na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Kusini mwa Afrika (SADC) ili kurahisisha ulinganifu katika jumuiya tunapoelekea kwenye muungano wa kifedha.

 

  1. Sababu za Kufanya Marejeo na Mabadiliko yanayotarajiwa

FBT zinafanyiwa marejeo ili kuakisi mienendo halisi ya matumizi ya kaya kwenye bidhaa na huduma mbalimbali. Marejeo ya FBT huhusisha mambo yafuatayo:-

  • Mabadiliko ya mizania (weights);
  • Kapu la bidhaa na huduma zinazotumiwa kukokotoa FBT;
  • Uhuishaji wa maeneo yanayotumika kukusanya bei za bidhaa na huduma mbalimbali zinazotumika katika ukokotoaji wa FBT,
  • Uboreshaji wa methodologia zinazotumika kukusanya bei za bidhaa na huduma za jamii, Mfano, NBS inatarajiwa kukusanya taarifa za bei za bidhaa na huduma kwa kutumia vishikwambi (tablets) badala ya madodoso ya karatasi kama ilivyokuwa awali;
  • Pamoja na hayo, miongozo ya kimatafa inaelekeza FBT zianze kutumia mchanganuo mpya wa matumizi ya kaya, yaani (Classification of Individual Consuption by Purpose, 2018(COICOP,2018) kutoka COICOP,1999. Mchanganuo huu ni mwongozo wa kimataifa uliokubaliwa kutumika na mataifa yote duniani. Mwongozo huu unaakisi mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia yaliyotokea duniani na ni wakilishi kwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea; na
  • Maboresho hayo hupelekea pia mabadiliko na uboreshaji wa programu ya compyuta (softwear) inayotumika kukokotoa FBT

 

  1. Vyanzo vya Taarifa Zinazotumika

Chanzo kikuu cha taarifa za matumizi ya kaya zinazotumika kuhuisha FBT ni Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa mwaka 2017/18 (HBS). Aidha vyanzo mbalimbali vya takwimu hutumika pamoja na HBS ili kuongeza uwakilishi wa matumizi ya kaya kwenye bidhaa na huduma mbalimbali. Vyanzo hivi ni Pamoja na takwimu za Pato la Taifa, hesabu za mwaka za makampuni mbalimbali, takwimu za kiutawala za uingizaji bidhaa nchini, bima, bidhaa za mtumba pamoja na matumizi ya wageni yaliyofanyika nchini.

 

  1. Maendeleo ya Uhuishaji wa FBT

Maandalizi ya uhuishaji wa FBT nchini yalianza mnamo mwezi Julai, 2020 kwa kuunda Kamati ya Kiufundi inayohusisha wadau muhimu wa FBT, wakiwemo NBS, Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu, Taasisi za Utafiti, Vyuo vya elimu ya juu, Wizara nyingine pamoja na Idara mbalimbali za Serikali. Jukumu kuu la kamati hii ni kutoa ushauri na miongozo ya kitaalamu ili kuhakikisha utekelezaji wa kazi hii unazingatia viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa. Mpaka sasa, NBS kwa kushirikiana na wadau wa FBT imekamilisha kazi zifuatazo:- ukokotoaji wa mizania ya FBT kutokana na matokeo ya utafiti wa HBS wa mwaka 2017/18 pamoja vyanzo vingine; kubadili mpangilio wa matumizi ya kaya kwenye bidhaa na huduma kutoka COICOP-1999 kwenda COICOP-2018 na Uandaaji wa Kapu la Bidhaa na Huduma mbalimbali zinazoakisi matumizi ya sasa. Pamoja na hayo, NBS inashirikiana kwa ukaribu wataalamu kutoka Jumuiya ya Afrika Mashiriki ili kuongeza uwazi na ubora katika zoezi hili.

 

  1. Ukamilishaji wa Uhuishaji wa FBT

NBS imepanga kuanza kutoa matokeo ya FBT mpya pamoja na Mfumuko wa Bei wa Taifa (MBT) mwanzoni mwa Januari, 2020. Tarehe halisi itaamuliwa baadaye kwa kuzingatia tarehe ya sasa, ambapo takwimu hizi hutolewa kila tarehe 8 ya mwezi unaofuata. Ili kufikia lengo hili, NBS kwa kushirikiana na wadau wa FBT imepanga kukamilisha kazi zifuatazo:-

  • uandaaji wa maeneo ya kukusanyia bei kwa ajili ya FBT mpya;
  • uandaaji wa mwongozo wa FBT kwa kuzingatia mabadiliko yaliyotokea; kubainisha sifa za bidhaa na huduma zitakazotumika katika ukokotoaji wa FBT;
  • uandaaji wa programu ya kukusanya bei kwa kutumia vishikwambi;
  • kufanya mafunzo ya wadadisi na wasimamizi juu ya mabadiliko ya FBT;
  • ukusanyaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi wa kizio;
  • ukokotoaji wa FBT kwa kutumia vigezo vilivyohuishwa na utangazaji wa FBT mpya.

 

Ofisi ya Taifa ya Takwimu inawaomba wananchi wote waendelee kutoa ushirikiano kwa Ofisi za Takwimu za Mikoa ili kufanikisha zoezi hili muhimu.

 

Ahsanteni.

 

Kwa mawasiliano zaidi tafadhali wasiliana na:    

 

Mtakwimu Mkuu wa Serikali,

Ofisi ya Taifa ya Takwimu,

Barabara ya Jakaya Kikwete,

S.L.P. 2683,

Dodoma,

TANZANIA.

 

Simu:           +255 26 -2963822,                                

Nukushi:      +255 26 -2963828,

Barua pepe:  This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.;                                       

Tovuti:         www.nbs.go.tz.