TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA KUADHIMISHA SIKU YA TAKWIMU AFRIKA

 

Tanzania kesho itaungana na nchi nyingine barani Afrika kuadhimisha Siku ya Takwimu Afrika ambayo kwa kawaida huadhimishwa tarehe 18 Novemba ya kila mwaka. Hapa Tanzania siku hiyo huadhimishwa tarehe 20 Novemba ya kila mwaka. Hata hivyo, kwa mwaka huu, kwa kuwa tarehe hiyo iliangukia siku ya Sherehe za Maulid, Maadhimisho hayo yatafanyika kesho tarehe 22 Novemba, 2018.

Lengo la Maadhimisho hayo ni kuongeza na kuimarisha uelewa wa wananchi wa bara la Afrika kuhusu umuhimu na nafasi ya takwimu katika maendeleo yao ya Kiuchumi na Kijamii. Kwa hivyo, kupitia Maadhimisho haya Ofisi ya Taifa za Takwimu za nchi za Afrika kuandaa programu mbali mbali za kutoa elimu na kuhimiza umuhimu wa Takwimu na matumizi yake kwa wananchi halikadhalika parogramu za wataalamu katika tasnia ya takwimu kuzungumzia masuala mbalimbali yahusuyo tasnia hiyo ikiwemo mafanikio na changamoto zake.

Chimbuko la Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika linatokana na uamuzi uliochukuliwa mwaka 1990 kwa pamoja na Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika na Mkutano wa pamoja wa watakwimu, wataalamu wa mipango na wataalamu wa idadi ya watu wa Afrika.

Katika Maadhimisho hayo kila mwaka kunakuwepo na kaulimbiu ambayo lengo lake ni kuweka msisitizo au kipaumbele katika moja ya maeneo muhimu ya kitakwimu mintarafu maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wananchi wa Nchi za Bara la Afrika.  

Kwa mwaka 2018, kaulimbiu ni Takwimu Rasmi Zenye Ubora Kuimarisha Uwazi, Utawala bora na Maendeleo Jumuishi (Highly Quality Official Statistics to Ensure Transparency, Good Governance and Inclusive Development).

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashattu Kijaji atakuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo zitakazofanyika Chuo cha Mipango, Dodoma ambapo watakwimu kutoka Serikali Kuu na Taasisi zake, Serikali za Mitaa, Vyuo vikuu na taasisi za kitafiti pamoja na wadau wengine watahudhuria sherehe hizo.

Imetolewa na;

Mtakwimu Mkuu wa Serikali

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU

DODOMA