Serikali yazindua Matokeo ya Utafiti wa Tathmini ya utoaji wa Huduma za Afya nchini wa mwaka 2014/2015

SERIKALI imesema imejipanga kuboresha huduma za Afya nchini ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za Afya zenye ubora na kwa wakati.

Akizungumza katika Uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Tathmini ya utoaji wa huduma za Afya nchini wa Mwaka 2014/2015, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangala amesema Serikali inajivunia huduma za Afya zinazotolewa hapa nchini japokuwa bado kuna changamoto ambazo serikali inaendelea kuzitafutia ufumbuzi.

1 a4ad5

“Serikali imejipanga kuhakikisha huduma za Afya zinapatikana kwa ubora na kwa wakati kwa wananchi wote ili Sekta ya Aya iendelee kuchangia katika ukuaji wa uchumi hapa Nchini. Leo tunazindua utafiti huu wa kutathmini utoaji wa huduma za Afya nchini wa mwaka 2014/2015, na matokeo yanaonesha kuwa huduma za Afya zimekuwa bora” “Mfano, utafiti unaonesha asilimia 80 ya vituo vyote vya Afya nchini vinatoa huduma za kisasa za uzazi wa mpango ikilinganishwa na takwimu zilizokusanywa katika utafiti kama huu wa mwaka 2006 ambapo ilikuwa ni asilimia 76 pekee,” amesema Kingwangala.

Kingwangala amesema utafiti pia unaonesha karibu vituo vyote vya Serikali, asilimia 97 vinatoa huduma za uzazi wa mpango ikilinganishwa na asilimia 35 ya vituo binafsi na asilimia 41 ya vituo vinavyomilikiwa na asasi za kidini. Amesema sekta ya Afya imeonesha kupata mafanikio makubwa katika kuhakikisha huduma za Afya nchini zinakuwa bora zaidi na hivyo kupitia Wizara yake wataendelea kufanya juhudi za dhati ili kutatua changamoto ambazo bado zinaikabili sekta ya Afya. Lengo la utafiti huu wa huduma za Afya ni kupata takwimu zitakazowezesha kuboresha utoaji wa huduma za Afya na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa. Aidha, utafiti huu ulijikita katika kuangalia Afya ya mama na mtoto, Afya ya mama mjamzito na mtoto aliyezaliwa, uzazi wa mpango, magonjwa yanayoambukizwa kwa kujamiana kama vile UKIMWI. Vilevile utafiti ulihusisha magonjwa ya kifua kikuu, malaria na magonjwa yasiyoambukizwa kama vile shinikizo la damu, kisukari na moyo.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dr. Albina Chuwa amesema utafiti huu ni wa pili tokea nchi ipate uhuru ambapo utafiti kama huu ulifanyika mwaka 2006 kwa lengo la kutathmini upatikanaji na utoaji wa huduma za Afya nchini.

2 b4951

“Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeweza kuendesha utafiti huu muhimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kuendesha utafiti huu katika vituo vyote vya Afya, Zahanati, Hospitali zinazomilikiwa na Serikali au watu binafsi na mashirika ya dini”

Utafiti huu ni muhimu katika kuisaidia Serikali, watunga sera na wadau mbalimbali wa maendelo katika kupanga na kupima utekelezaji wa mipango mbalimbali ya utoaji na uboreshaji wa huduma za Afya nchini,” amesema Dr. Chuwa.

Dr. Chuwa amesema utafiti unaonesha utoaji wa huduma za Afya umekuwa bora ukilinganisha na mwaka 2006 ulipofanyika utafiti wa awali ambapo hivi sasa takribani vituo vyote vinatoa huduma ya kupima Malaria kwa kutumia aidha kipimo cha ‘RTD’ au ‘Microscopy’.

Aidha ameongeza kuwa, asilimia 81 ya vituo vyote vya Afya nchini vinatoa huduma ya kupima Virus vya UKIMWI ikiwa ni asilimia 96 kwa hospitali, vituo vya afya kwa asilimia 92 na zahanati kwa asilimia 80.Utafiti pia unaonesha bado kuna changamoto kadhaa katika utoaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, vyoo na umeme ambavyo vinahitaji kutafutiwa ufumbuzi.Utafiti wa kutathmini utoaji wa huduma za Afya nchini wa Mwaka 2014/2015 uliojumuisha Tanzania bara na Zanzibar, ambao umedhaminiwa na Serikali ya Tanzania, Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo la USAID, pia umechangiwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Serikali ya Uingereza la DFID, Serikali ya CANADA na Benki ya Dunia.

3 557c8

Takwimu na taarifa zilizokusanywa katika utafiti huu zitatumika kuboresha mikakati mipya na kuboresha mfumo wa afya uliopo hapa nchini.