The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Buehren: Tathmini ya NSS Itatoa Nafasi kwa Wadau wa Sekta ya Takwimu Kukuza Matumizi ya Teknolojia
Posted On: 28 January, 2026
Buehren: Tathmini ya NSS Itatoa Nafasi kwa Wadau wa Sekta ya Takwimu Kukuza Matumizi ya Teknolojia

Mchumi Mwandamizi, Benki ya Dunia Tanzania, Niklas Buehren, kwa niaba ya Mratibu wa Timu ya Utekelezaji ya Benki hiyo kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Takwimu Kanda ya Mashariki mwa Afrika, Dhiraj Sharma amesema kuwa mchakato wa tathmini ya Mfumo wa Taifa wa Takwimu (National Statistical System – NSS) utatoa nafasi kwa wadau wa sekta ya takwimu nchini kukuza matumizi ya teknolojia hasa matumizi ya teknolojia za kisasa kama Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI).
Buehren ameyasema hayo alipokuwa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mchakato wa tathmini ya Mfumo huo, iliofanyika kwenye Ukumbi wa Ngorongoro uliopo katika jengo la makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma tarehe 27 Januari 2026 ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Usimamizi wa Fedha za Umma, Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba.
Amesema tathmini hiyo itawezesha wadau wa takwimu kujiangalia kwa ujasiri na kwa uwazi, kutambua maeneo yanayofanya kazi vizuri, yale yanayohitaji maboresho, pamoja na fursa mpya zinazojitokeza, hususan katika teknolojia hiyo imekuwa sehemu isiyoweza kuepukika katika uzalishaji, uchambuzi, usambazaji na utumiaji wa takwimu husika.

Buehren amehitimisha kwa kusema kuwa tathmini ya Mfumo wa Taifa wa Takwimu itakuwa fursa muhimu ya kuimarisha uhusiano kati ya wazalishaji na watumiaji wa takwimu, na kuhakikisha data zinatumika ipasavyo katika kupanga na kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.