Historia
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ilianzishwa kama Wakala wa Serikali tarehe 26 Machi, 1999 kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa Serikali Na. 30 ya Mwaka 1997. Kabla ya hapo, NBS ilijulikana kama Idara Kuu ya Takwimu iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Takwimu Sura 443 ya Mwaka 1961 (Statistical Ordinance Cap. 443 of 1961). Sheria hii ilitungwa mara tu baada ya kupata Uhuru. Aidha, Sheria hii ilifuta Sheria ya Takwimu ya Mwaka 1949 (Statistical Ordinance of 1949- Chapter 443) ambayo ilikuwa ikitumika katika nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania chini ya utawala wa kikoloni wa Uingereza.
Ikiwa kama Wakala wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Takwimu iliendelea kutekeleza majukumu yake kwa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 1961 (The Statistics Ordianance) hadi ilipofutwa kwa Sheria ya Takwimu Na.1 ya Mwaka 2002 ambayo ililenga kuimarisha na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za kitakwimu na uratibu wa mfumo mzima wa taifa wa uzalishaji na usambazaji takwimu nchini.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu iliundwa upya na kuwa taasisi inayojitegemea kupitia Sheria ya Takwimu Na. 9 ya Mwaka 2015 yaani Sheria ya Takwimu Sura 351 (Marejeo ya Mwaka 2019). Kutokana na mabadiliko hayo NBS imepewa majukumu ya kukusanya, kuzalisha na kusambaza takwimu rasmi nchini pamoja na kuratibu Mfumo wa Taifa wa Takwimu nchini.
DIRA
Kuwa kitovu cha takwimu rasmi Tanzania.
DHAMIRA
Kutoa takwimu rasmi zilizo bora na huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kupanga mipango na kufanya maamuzi yenye uthibitisho.