CGS Ali: Mapitio ya Mifumo Yanaimarisha Uratibu, Ufanisi Sekta ya Takwimu
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Kassim Salum Ali, amesema Tanzania imekuwa ikifanya mapitio ya mifumo ya takwimu mara kwa mara tangu mwaka 1973, hatua inayosaidia kuimarisha uratibu na ufanisi wa sekta ya takwimu kwa kipindi kirefu.
Ali ameyasema hayo alipokuwa akifunga hafla ya uzinduzi wa mchakato wa tathmini ya Mfumo wa Taifa wa Takwimu (National Statistical System – NSS), iliofanyika kwenye Ukumbi wa Ngorongoro uliopo katika jengo la makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma tarehe 27 Januari 2026 ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Usimamizi wa Fedha za Umma, Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba
Kiongozi huyo amesema tathmini zilizopita, ikiwemo tathmini ya Mpango wa Maendeleo ya Takwimu wa Taifa - TSMP I, zilitoa msingi muhimu wa kuandaa TSMP II, licha ya tathmini hiyo kufanyika ndani ya maeneo mahususi kama takwimu za kijinsia na siyo mfumo mzima kwa ujumla.
Aidha, amehitimisha kwa kusema kuwa lengo kuu la tathmini hiyo ni kuhakikisha matokeo na mapendekezo yatakayotolewa yanatekelezeka kwa vitendo na yanasaidia kuimarisha ufanisi na uimara wa Mfumo wa Taifa wa Takwimu nchini.
Mchakato wa tathimini hiyo unahusisha taasisi za serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, wazalishaji na watumiaji wa takwimu, watunga sera, washirika wa maendeleo na wananchi kwa ujumla.