Chemba Yafikiwa, Wadadisi Utafiti wa Kilimo
Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS inaendelea na zoezi la Utafiti wa Kilimo wa Mwaka 2024/2025 unaofanyika kote nchini, ambao una lengo la kukusanya takwimu kuhusu ukubwa wa maeneo ya kilimo na uzalishaji wa mazao, idadi ya mifugo na mazao yatokanayo na mifugo pamoja na ufugaji wa viumbe maji.
Zoezi hilo linahusisha ukusanyaji wa taarifa kutoka kwa wakulima na wafugaji kuhusu aina ya mazao wanayolima, mifugo wanayofuga, ukubwa wa mashamba, ufugaji wa nyuki na ukuzaji wa viumbe maji pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo katika shughuli zao za kilimo.
Akizungumza akiwa katika Kitongoji cha Mialo, Kijiji cha Mialo, Kata ya Kwamtoro, Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma wakati wa zoezi hilo tarehe 02 Februari 2026, Mtakwimu ambaye ni Msimamizi wa Timu ya Utafiti huo Wilaya ya Chemba, Unambwe Erasto Mungure amesema kuwa zoezi hilo ni muhimu katika kuhakikisha Serikali inapata takwimu sahihi zitakazosaidia kufanya maamuzi yenye tija katika sekta ya kilimo.
Aidha, Mtakwimu huyo amesisitiza kuwa kilimo ni uti wa mgongo kwani kwa mujibu wa Takwimu za Pato la Taifa Tanzania Bara za Mwaka 2018 – 2024, kilimo kinakuwa kwa takriban asilimia 4 na kinachangia Pato la Taifa kwa asilimia 26 na kwa upande wa ajira, imeajiri asilimia 61 ya Watanzania ambapo, takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa sekta ya kilimo nchini.
Pia, Mungure ameeleza kuwa zoezi hilo limekuwa na mwitikio mzuri kwani Wananchi wanatoa ushirikiano hali ambayo itasaidia kutoa viashiria vya msingi kwa ajili ya maendeleo ya hiyo.
Hamidu Mustapha Maulid ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mialo, yeye ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kufanya utafiti huo kwani utaisaidia Serikali kupanga mipango madhubuti ya kuboresha sekta ya kilimo nchini.
Maulid ameongeza kuwa Utafiti huo, utasaidia kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ambapo amewaomba Wananchi wanaotembelewa na wadadisi kutoa ushirikiano na kuwaasa Wananchi kutoa taarifa sahihi kwa ajili ya kuisaidia Serikali katika kuboresha kilimo nchini