Dkt. Minja Awataaka Wadadisi, Wasimamizi Kuwa Waadilifu
Wadadisi 150 na wasimamizi wa zoezi la Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2026, wameaswa kuwa waadilifu wakati wote wa utekelezaji wa zoezi la ukusanyaji wa taarifa za utafiti huo ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni nchini kote.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi ya Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Dkt. Ruth Minja alipokuwa akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Mount Uluguru Morogoro mjini tarehe 09 Februari 2026.
Dkt. Minja amewakumbusha Wataalam hao kuzingatia kuwa taarifa zitakazo kusanywa ni muhimu kwa Serikali kwani zitasaidia kupata Takwimu za watu wenye uwezo wa kufanya kazi ili kuiwezesha kutoa ajira, kuunda na kutathmini sera mbalimbali zinazohusiana na soko la ajira.
"Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa Wananchi katika kaya mbalimbali zitakazohusishwa katika utafiti huu, kutoa ushirikiano kwa wadadisi na Wataalam wa NBS ili kupata Takwimu sahihi kwa manufaa ya Taifa letu." Amesema Dkt. Minja
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Ofisi ya Taifa ya Takwimu Wakili Oscar Mangula amewaapisha Wadadisi hao kwa ajili ya kwenda kukusanya taarifa katika Utafiti huo kutoka kwa Wananchi watakaofikiwa.
Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi hufanyika mara nne kwa mwaka ambapo kwa mwaka 2026, Awamu ya Kwanza ya Utafiti huo inafanyika kuanzia mwezi Februari hadi Machi.