The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Dkt. Msengwa: Maendeleo ya Teknolojia Kichocheo Kasi ya Mabadiliko Ukusanyaji, Uchambuzi, Usambazaji wa Takwimu
Posted On: 28 January, 2026
Dkt. Msengwa: Maendeleo ya Teknolojia Kichocheo Kasi ya Mabadiliko Ukusanyaji, Uchambuzi, Usambazaji wa Takwimu

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema maendeleo ya teknolojia ya kidijitali ni kichocheo cha kasi ya mabadiliko ya ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa takwimu, hivyo kufanya tathmini ya Mfumo wa Taifa wa Takwimu (National Statistical System – NSS) ni fursa ya kuhakikisha mfumo wa taifa unaendana na mabadiliko ya kiteknolojia na ubunifu wa kisasa.
Dkt. Msengwa ameyasema hayo alipokuwa akitoa utangulizi wakati wa hafla ya uzinduzi wa mchakato wa tathmini ya Mfumo huo, iliofanyika kwenye Ukumbi wa Ngorongoro uliopo katika jengo la makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma tarehe 27 Januari 2026 ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Usimamizi wa Fedha za Umma, Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba.
Dkt. Msengwa ameongeza kuwa matokeo ya tathmini hiyo yataongoza maandalizi ya mpango mkakati ujao yaani Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Takwimu Awamu ya Tatu (TSMP III) pamoja na mikakati ya utekelezaji wake kwa mtazamo wa mbele.wa sekta ya takwimu, ambao utaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na vipaumbele vya kitaifa katika kupanga na kutekeleza sera zinazotegemea ushahidi wa takwimu.

Kiongozi huyo ameeleza kuwa Mfumo wa Taifa wa Takwimu ni mpana na haujumuishi tu Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS au Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar - OCGS, bali pia unahusisha taasisi za serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, wazalishaji na watumiaji wa takwimu, watunga sera, washirika wa maendeleo na Wananchi kwa ujumla.

“Viongozi wa kitaifa, wawekezaji, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo wanategemea takwimu rasmi zilizo sahihi na zinazoaminika ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali na kutumia fursa zilizopo.” Amesema Dkt. Msengwa na kuongeza;

“Ndiyo maana leo tunatazama kwa pamoja jinsi mabadiliko ya haraka ya teknolojia yanavyobadilisha shughuli zetu za kila siku, kuanzia uzalishaji hadi matumizi ya takwimu, lengo letu leo ni kuona namna tunaweza kubuni, kuboresha na kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia ya sasa.”

Dkt. Msengwa ametoa shukrani kwa wadau wote wa sekta ya takwimu nchini kwa ushiriki wao, kwani anaamini ushirikiano wa wadau hao ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo imara wa takwimu unaojibu mahitaji ya maendeleo ya taifa la Tanzania.

Kadhalika, Kiongzi huyo ameishukuru Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya kwa mchango wao wa kifedha na kitaalamu, akibainisha kjuwa ushirikiano huo umeendelea kuimarisha uwezo wa Tanzania katika uzalishaji, usambazaji na matumizi ya takwimu rasmi zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.