Dkt. Ruzegea Afungua Mkutano wa 52 wa Wakutubi, Awataka kuwa Walinzi Taarifa za Faragha
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania – TLSB, Dkt. Mboni Ruzegea amefungua rasmi Mkutano wa 52 wa Chama cha Wakutubi Tanzania – TLA unaofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Rock City Mall jijini Mwanza tarehe 09 Februari 2026 ambapo amewataka Wahutubi kote nchini kuwa walinzi wa taarifa za faragha hususan katika zama hizi za kidijitali.
Dkt. Ruzegea, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa maktaba za leo si mahali pa kuhifadhi vitabu pekee, bali zimegeuka kuwa vituo hai vya maarifa vinavyotumia teknolojia za kisasa kuwezesha ujifunzaji, utafiti na ubunifu.
Akizungumza katika Mkutano huo wenye kauli mbiu “Reimagining Libraries in the Digital Age, Empowering Communities, Advancing Knowledge and Driving Innovation”, amesema kuwa mabadiliko ya kidijitali yamewapa wakutubi majukumu mapya yakiwemo usimamizi wa mifumo ya kidijitali, ulinzi wa taarifa na uelimishaji wa jamii katika matumizi sahihi ya taarifa.
Kiongozi huyo amesema ulinzi wa faragha na usalama wa taarifa ni suala nyeti katika zama za kidijitali, hasa kutokana na ongezeko la matumizi ya maktaba za mtandaoni, hifadhi za kitaasisi na majukwaa ya kujifunzia mtandaoni. Aidha, wakutubi wana nafasi muhimu katika mapambano dhidi ya taarifa potofu, habari za kupotosha na za uongo kupitia elimu ya habari kwa jamii.
Amesema Serikali inaendelea kutambua na kuthamini mchango wa wakutubi katika kuimarisha elimu, utafiti na ujenzi wa jamii yenye maarifa, huku akitaja changamoto zinazoikabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na miundombinu duni ya TEHAMA, gharama za mifumo ya kidijitali na upungufu wa rasilimali watu wenye ujuzi wa kidijitali.
Dkt. Ruzegea amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika mafunzo na programu za kuwajengea uwezo wakutubi ili waendane na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na kuendelea kuwa chachu ya maendeleo ya jamii na uchumi wa maarifa wa Taifa.
Baada ya Ufunguzi wa Mafunzo hayo Mkurugenzi Dkt. Ruzegea alitembelea Banda la Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS lilipo nje ya Ukumbi huo ambapo alipata fursa ya kukutana na Wakutubi wabobezi ambao walimuelezea majukumu ya Ofisi hiyo ikiwemo jukumu kuu la kukusanya, kuchakata na kusambaza Takwimu kjwa Taasisi za Umma, Vyuo, Watafiti, Wadau wa Maendeleo na Wananchi ili ziweze kutumika katika mipango mbalimbali ya maendeleo.
Mkutano huo wa siku tano (tarehe 09 hadi 13 Februari 2026) unawashirikisha Wakutubi kutoka Sekta za Umma na Binafsi.