The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Luswetula Azindua Bodi ya NBS
Posted On: 24 February, 2026
Luswetula Azindua Bodi ya NBS

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) amezindua Bodi ya Tatu ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, akimuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro uliopo Jengo la Takwimu Makao Makuu ya Ofisi hizo jijini Dodoma tarehe 23 Februari 2026.

Mhe. Luswetula amewataka Wajumbe wa Bodi hiyo kutekeleza kikamilifu majukumu yao kwa kuzingatia Sheria ya Takwimu Sura ya 351 ambapo amefafanua kuwa NBS ni Ofisi muhimu kwani Takwimu zinazozalishwa na Ofisi hiyo ni muhimu kwa Serikali kwani zinatumika kutunga sera, kupanga mipango na utoaji wa maamuzi sahihi ya maendeleo endelevu.

“Napenda kutumie nafasi hii kukupongeza wewe Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi kwa kuaminiwa na kuteuliwa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu...sote tunafahamu Taasisi hii ni nyeti na ya kimkakati hivyo mtambue kuwa mmeaminiwa na kupewa jukumu kubwa na hamna budi kuilinda imani hiyo. Amesema Mhe. Luswetula na kuongeza;

“Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Sote ni mashuhuda kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuhakikisha upatikanaji wa takwimu rasmi kwa ajili ya kuiwezesha Serikali na wadau wengine kufanya maamuzi yenye ushahidi wa kitakwimu, ambayo yanakuwa na tija zaidi na yanayoakisi hali halisi ya mahitaji ya Wananchi.”

Aidha, Mhe. Luswetula amesema Takwimu zinazoratibiwa na Ofisi ya hiyo ni msingi wa kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mipango ya Taifa ya Maendeleo ya miaka mitano pamoja na Mipango ya kisekta.

Amesema Takwimu rasmi ndizo zinazowezesha ulinganifu wa Tanzania kimataifa na kikanda katika utekelezaji wa ajenda za pamoja kama vile Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030 na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika ya Mwaka 2063.

Kiongozi huyo amewataka Wajumbe wa Bodi kuweka kipaumbele katika kuimarisha utendaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Takwimu na ushiririkiano wa sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia upatikanaji wa Takwimu rasmi nchini.

Kadhalika, Mhe. Luswetula amewasisitiza Wajumbe hao kutumia fursa za teknolojia zilizopo kuongeza ufanisi wa uzalishaji na usambazaji wa takwimu rasmi ili kupunguza pengo la takwimu lililopo katika sekta mbalimbali. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mhe. Anne Semamba Makinda, amesema bodi hiyo itaendelea ushirikiana kwa karibu na Menejimenti ili kuhakikisha uzalishaji wa takwimu rasmi unaimarika na kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Mhe. Makinda amesema kupitia weledi na uzoefu wa wajumbe wa bodi, taasisi hiyo itaweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga na kufanya maamuzi yenye ushahidi.

Akizungumza awali Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mhe. Anne Semamba Makinda kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya NBS ambapo amesema Ofisi hiyo imejithatiti katika kuboresha na kusimika mifumo ya teknolojia ya kisasa ili kuendana na wakati.