The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Malima: Hakikisheni Viwango Hivi Vinaendelea Kupanda
Posted On: 22 December, 2025
Malima: Hakikisheni Viwango Hivi Vinaendelea Kupanda

Mkuu wa Mkoa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kwa utendaji mzuri uliojikita kutimiza malengo ya kukusanya, kuchakata na kutoa Takwimu bora zenye viwango vinavyokubalika katika vigezo vya kitaifa na kimataifa.

Mhe. Malima ametoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza wakati wa hotuba yake katika  Mkutano wa Pili wa Baraza la Saba la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo, lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Cate, mkoani Morogoro tarehe 18 na 19 Disemba 2025.

“Nakiri kuwa Ofisi yangu ni mnufaika mkubwa wa Publications (Machapisho) zenu, the work ethics is different (maadili ya utendaji kazi yamebadilika)...nina utajiri wa taarifa, ninapofanya kazi zangu, sibabaishi kuhusu ubora wa takwimu ninazozipata kutoka NBS...hivyo hongereni sana ila niwasisitize kudumisha viwango bora vya takwimu vilivyofikiwa, kwa kuwa takwimu hizo zina mchango wa moja kwa moja katika jamii.” Amesema RC Malima.  

Aidha, Mhe. Malima ameipongeza NBS kwa kuzingatia umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi katika kuhamasisha namna ya upatikanaji wa haki za wafanyakazi, ushiriki na ushirikishwaji wa wafanyakazi katika masuala mbalimbali yanayohusu uongozi, utawala na utekelezaji wa majukumu ya taasisi katika kuchangia maendeleo sehemu ya kazi.

‘’NBS imekuwa mfano bora katika utekelezaji wa sheria na kanuni zinazounda mabaraza ya Wafanyakazi, sina shaka yoyote kuwa Menejimenti na Wafanyakazi wanatambua umuhimu wa Baraza na namna vikao hivi vinavyochangia utekelezaji wa malengo ya taasisi. Ni dhahiri kuwa haya yamewezekana kutokana na kuwepo kwa mawasiliano na ushirikiano chanya kati ya menejimenti na TUGHE.’’ Amesema Mhe. Malima.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amesema Baraza la Wafanyakazi limeendelea kuwa chombo muhimu cha mshikamano, uwazi na ushirikishwaji ndani ya taasisi kupitia majadiliano na vikao mbalimbali.

Akieleza majukumu ya NBS, Dkt. Msengwa amesema kuwa Ofisi hiyo inaendelea kufanya sensa mbalimbali ikiwemo Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Viwanda, Sensa za Kilimo na Tafiti za Kijamii, Kiuchumi na Mazingira.

Pia, Dkt. Msengwa amesisitiza kuwa Takwimu zinazozalishwa na NBS zimekuwa msingi wakutunga sera na mipango ya maendeleo nchini na zimeendelea kuimarisha nafasi ya NBS kama taasisi ya kitaifa yenye kuaminika katika kuzalisha takwimu sahihi, rasmi na zenye ubora kimataifa.

Naye, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda amewahimiza wafanyakazi wa NBS kuwasililisha kwa menejimenti changamoto zinazowakabili ili ziweze kutatuliwa na amewahasa kudumisha utamaduni wa kujaliana, kupendana na kufanya kazi kwa umoja.

‘’Napenda tuwe na taasisi yenye furaha, uadilifu, uhodari, taasisi ambayo imeonekana duniani kwamba ni taasisi kweli ya takwimu kitaifa na kimataifa.’’ Amesema Mhe. Makinda.

NBS imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi wake na kuendeleza majadiliano yenye tija kupitia Baraza la Wafanyakazi, hatua inayochangia kuongeza ufanisi wa kazi, uwajibikaji na utoaji wa Takwimu sahihi zitakazo saidia kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya Taifa.