Mhe. Makinda: Tathmini ya Nss Itasaidia Kutekeleza DIRA 2025
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda amesema mchakato wa tathmini ya Mfumo wa Taifa wa Takwimu (National Statistical System – NSS) unafanyika katika kipindi muafaka, kwani kwa sasa Tanzania inaendelea na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Mhe. Makinda ameyasema hayo alipokuwa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mchakato wa tathmini ya Mfumo huo, iliofanyika kwenye Ukumbi wa Ngorongoro uliopo katika jengo la makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma tarehe 27 Januari 2026 ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Usimamizi wa Fedha za Umma, Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba.
Mchakato huo unalenga kuifikisha Tanzania katika hadhi ya nchi ya kipato cha kati cha juu ifikapo Mwaka 2050, huku takwimu sahihi na kwa wakati zikiwa nguzo muhimu ya kufanikisha malengo hayo.
Aidha, Mhe. Makinda amefafanua kuwa zoezi hilo linalenga kuchambua kwa kina ubora na ukomavu wa Mfumo wa Taifa wa Takwimu, kubaini changamoto zilizopo na fursa zinazojitokeza, pamoja na kutoa mapendekezo yatakayosaidia maboresho ya mfumo huo.
Kiongozi huyo, ameongeza kuwa tathmini hiyo itahusisha mapitio ya mfumo wa kisheria, uwezo wa rasilimali watu, mbinu za ukusanyaji na uchambuzi wa data, matumizi ya teknolojia na vyanzo vipya vya data, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya wazalishaji na watumiaji wa takwimu.