Naibu Katibu Mkuu Shaaban Azindua Rasmi Mchakato wa Tathmini ya NSS
Naibu Katibu Mkuu Usimamizi wa Fedha za Umma, Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban amezindua rasmi mchakato wa Tathmini ya Mfumo wa Taifa wa Takwimu (National Statistical System – NSS) akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Ngorongoro uliopo katika jengo la makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma tarehe 27 Januari 2026.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar - OCGS imezindua rasmi mchakato huo ikiwa ni hatua muhimu inayolenga kuimarisha uzalishaji, ubora na matumizi ya takwimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, kiongozi huyo amesema kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi, kwa wakati na kwa urahisi ni nguzo muhimu ya utawala bora, upangaji wa sera na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Takwimu sahihi, kwa wakati na zinazopatikana kwa urahisi si namba tu kwenye ripoti, bali ni msingi wa kujenga sera, kupima maendeleo na hatimaye kuboresha maisha ya kila Mtanzania.” Amesema Shaaban.
Kiongozi huyo amesema tathmini ya NSS inalenga kuchambua kwa kina utendaji wa mfumo mzima wa takwimu nchini, ikihusisha uzalishaji wa data, uratibu wa taasisi, ubora wa takwimu, matumizi ya teknolojia na usambazaji wa taarifa kwa watumiaji.
Amesema mchakato huo utaiwezesha Tanzania kubaini upungufu uliojitokeza katika uimarishaji wa NSS nchini kupitia miradi mbalimbali siku za nyuma, kujifunza njia sahihi na kubaini fursa zilizopo katika uimarishaji wa Mfumo huo kwa siku zijazo ambapo ameelekeza wdau wa Mfumo huo kutoa ushirikiano kwa Timu ya Wataalamu waelekezi watakaowatembelea taasisi zao kwa ajili ya kufanya majadiliano ya kina.
Shaaban amewatoa hofu wadau wote wa Mfumo huo kuwa tathmini hiyo siyo ukaguzi wa makosa, bali ni zoezi shirikishi la kubaini mafanikio, changamoto na fursa za kuimarisha zaidi Mfumo wa Takwimu wa Taifa.
Aidha, Kiongozi huyo ameipongeza NBS kwa kushika nafasi ya pili barani Afrika kwa ubora wa takwimu baada ya Afrika Kusini, kwa mujibu wa tathmini ya Benki ya Dunia kwa nchi 54 za Afrika kati ya mwaka 2006 hadi 2026.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya takwimu kupitia utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Takwimu Awamu ya Kwanza na ya Pili (TSMP I na II) nchini - zikiwa na mkazo mkubwa katika ulinganifu wa takwimu, ubora na usambazaji wa data, uzalishaji wa takwimu na miundombinu, pamoja na maendeleo ya taasisi.” Amesema Naibu Katibu Mkuu Shaaban na kuongeza;
“Niwahimize wadau wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hili ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo imara wa takwimu unaoaminika, unaowajibika na unaotumika kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.”