The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS Inaendelea, Utafiti wa Kilimo nchini
Posted On: 02 February, 2026
NBS Inaendelea, Utafiti wa Kilimo nchini

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS inaendelea na zoezi la Utafiti wa Kilimo wa Mwaka 2024/2025 unaofanyika kote nchini, ambao una lengo la kukusanya takwimu kuhusu ukubwa wa maeneo ya kilimo na uzalishaji wa mazao, idadi ya mifugo na mazao yatokanayo na mifugo pamoja na ufugaji wa viumbe maji.

Zoezi hilo linahusisha ukusanyaji wa taarifa kutoka kwa wakulima na wafugaji kuhusu aina ya mazao wanayolima, mifugo wanayofuga, ukubwa wa mashamba,  ufugaji wa nyuki na ukuzaji wa viumbe maji pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo katika shughuli zao za kilimo.

Akizungumza akiwa katika Kijiji cha Kisima cha Ndege, Kata ya Msisi, Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma wakati wa zoezi hilo tarehe 30 Januari 2026, Mtakwimu ambaye pia ni miongoni wa Wasimamizi wa Timu ya Utafiti huo Mkoa wa Dodoma, Nasriya Hussein Alli amesema kuwa zoezi hilo ni muhimu katika kuhakikisha Serikali inapata takwimu sahihi zitakazosaidia kufanya maamuzi yenye tija katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wake Mdadisi, Veronica Mwisomba amewashukuru Wananchi wa Kijiji hicho, kwa kuonyesha ushirikiano hasa ikizingatiwa kuwa utafiti huu unafanyika ikiwa ni msimu wa kilimo ambapo Wananchi wengu wanatumia muda mwingi katika shughuli za kilimo.

Richard Chiteto Lesilwa ni Mkulima na Mfugaji katika Kijiji hicho ambapo yeye ameipongeza na kuishukuru Serikali na kwamba anaamini taarifa anazozitoa zitaisaidia Serikali kuboresha huduma za kilimo na kutatua changamoto anazokutana nazo shambani.

Naye, Zacharia Mazengo ambaye ni Mkulima anayeshiriki kutoa taarifa katika utafiti huo amesema zoezi hilo ni fursa muhimu kwa wakulima katika kueleza changamoto zinazowakabili Wakulima ili ziweze kuzitatua na Serikali kwa wakati. Amesema ushirikishwaji huo wa Wananchi moja kwa moja unatoa matumaini ya maboresho katika sekta ya kilimo.

Aidha, Jerome Yohana Chiholo ambaye ni Mkulima katika Kitongoji cha Mikoroshini kijijini hapo amaeiomba Serikali kupitia utafiti huo kuboresha sekta ya kilimo kwa kuwa wanapitia changamoto za uhaba wa maji ya uhakika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, mbegu bora, dawa na viuatilifu mbalimbali, mbolea na maafisa ugani ili waweze kutoa huduma za usaidizi kwa wakulima.