The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS, OCGS Zahakiki Taarifa za Utafiti wa Mapato, Matumizi Kaya Binafsi
Posted On: 20 January, 2026
NBS, OCGS Zahakiki Taarifa za Utafiti wa Mapato, Matumizi Kaya Binafsi

Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar – OCGS kwa pamoja zimeendelea na zoezi la uhakiki na uhariri wa taarifa za Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania wa Mwaka 2025 uliofanyika kuanzia Januari hadi Disemba 2025 ambapo zoezi hilo linafanyika kwenye Ukumbi wa Four Points jijini Dar es Salaam kwa siku tano kuanzia tarehe 19 hadi 23 Januari 2026.

Akizungumza leo tarehe 20 Januari 2026 kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Meneja Idara ya Takwimu za Mazingira na Makazi Stephano G. Cosmas ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuridhia kufanyika kwa utafiti huu na kuziwezesha Ofisi za Takwimu kutekeleza Utafiti huo kupitia Mradi wa Mpango Kabambe wa Pili wa Maendeleo ya Takwimu nchini - TSMP II.

Aidha, Cosmas amewashukuru wadau wote wa utafiti huo pamoja na Wananchi walioshiriki kutoa taarifa wakati wa utafiti huo na kuwaomba kuendelea kutoa ushirikiano katika tafiti nyingine zinazofanywa na ofisi hizo.

Pia, ameongeza kuwa Ofisi hizo zitaendelea kufanya kazi pamoja kuhakikisha kuwa ripoti hiyo inakamilika kwa wakati ili kuziwezesha Serikali kupanga mipango inayoakisi takwimu za sasa.

Naye Meneja wa Takwimu za Idadi ya Watu na Matukio ya Kijamii – OCGS, Abdulmajid Jecha Ramadhan amesema matokeo ya Utafiti huo yatasaidia kupata viashiria mbalimbali vikiwemo vya kijamii, kiuchumi na vya kuonyesha hali ya umasikini Tanzania.

Jecha ameeleza kuwa viashiria vinavyotokana na utafiti huo vitasaidia Serikali katika kupanga mipango na sera mbalimbali zinazolenga kupunguza hali ya umasikini katika jamii nchini ikiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF, Sera ya Elimu Bure, Mikopo ya Elimu ya Juu kwa Wanafunzi na Bima kwa Wote.