The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS, TALIRI, WB kufanya Utafiti wa Kutafuta Njia Bora ya Ukusanyaji wa Taarifa za Mifugo
Posted On: 26 February, 2026
NBS, TALIRI, WB kufanya Utafiti wa Kutafuta Njia Bora ya Ukusanyaji wa Taarifa za Mifugo

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS, Dkt. Amina Msengwa amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania – TALIRI, Prof. Erick Vitus Komba ofisini kwake Makao Makuu ya NBS jijini Dodoma tarehe 25 Februari 2026, kwa lengo la kupanga mipango ya pamoja ili kutekeleza zoezi la Utafiti wa Kutafuta Njia Bora ya Ukusanyaji wa Taarifa za Mifugo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Utafiti huo ambao utafanyika kwa pamoja kati ya Taasisi hizo kwa kushirikia na Benki ya Dunia una lengo la kuangalia njia bora za kupata idadi ya ng’ombe pamoja na kiasi cha maziwa kinachozalishwa katika kaya ambazo zinajihusisha na ufugaji wa ng’ombe.

Viongozi hao kwa pamoja wamekubaliana kuwa Taasisi hizo zina wajibu wa kutekeleza zoezi hilo kwa ufanisi lengo likiwa ni kuboresha mbinu za ukusanyaji wa taarifa hizo katika ngazi ya kaya ili kuziba pengo la upatikanaji wa takwimu za kilimo na mifugo nchini.

Tanzania imechaguliwa kuwa ya mfano kati ya nchi 50 duniani ambazo ni mwana chama wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa – FAO ambazo zinashiriki katika Mkakati wa Kuboresha Takwimu za Kilimo ifikapo Mwaka 2030.

Ambapo matokeo ya utafiti huo yanategemewa kutumika katika nchi hizo ili kuboresha mbinu bora za ukusanyaji wa takwimu za mifugo (ng’ombe) pamoja na mazao yake yakiwemo maziwa.

Aidha, Kabla ya kuanza kwa Utafiti huo, tarehe 02 hadi 11 Machi 2026 yataanza mafunzo kwa wataalam wote watakaoshiriki katika zoezi hilo na kisha utafiti utafanyika kwa muda wa mwezi mmoja kwa awali ukihusisha mikoa miwili ya Arusha na Tabora.