The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS, TPDF, UDSM Zasaini Mkataba Utekelezaji Mradi wa MOWIP
Posted On: 12 February, 2026
NBS, TPDF, UDSM Zasaini Mkataba Utekelezaji Mradi wa MOWIP

Chief of Staff of The Tanzania People's Defence Forces (TPDF), Luteni Jenerali Salum Haji Othmani amesaini Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Kupima Fursa kwa Wanawake katika Oparesheni za Ulinzi wa Amani – MOWIP ambao umefadhiliwa na Mfuko wa Elsie Initiative (Elsie Initiative Fund – EIF) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa Wanawake Tawi la Tanzania (UN Women Tanzania).

Hafla hiyo fupi ya utiaji saini imefanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania – TPTC Kunduchi jijini Dar es Salaam tarehe 11 Februari 2026 ambapo lengo la Mradi huo wa MOWIP ni kuongeza ushiriki wa Wanawake katika Oparesheni za Ulinzi wa Amani pamoja na kuimarisha mifumo ya uongozi, usawa wa kijinsia na uwajibikaji ndani ya taasisi za kijeshi.

Aidha, ili kutekeleza Mradi huo, Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania - JWTZ, Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – UDSM kwa pamoja Chombo hicho kimesaini mkataba baina yake na taasisi hizo kufanya utafiti wa kubaini vikwazo vinavyoweza kuzuia ushiriki wa Wanawake katika Ulinzi wa Amani.

 Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Salum Haji Othmani ameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa utayari wa kushiriki utafiti huo ambapo amesema Jeshi hilo litatoa ushirikiano kwani limejidhatiti kujenga usawa jumuishi katika oparesheni za ulinzi wa amani.

“Ni matumaini yetu kwamba matokeo ya Utafiti huu yataongeza thamani hususan mchango wa Wanawake katika Oparesheni za Ulinzi wa Amani…tunaamini mradi huu utawawezesha Askari Wanawake wa Jeshi hili kujengewa uwezo kwa njia ya mafunzo ambayo yatawawezesha kupata ujuzi, ufahamu na kutambua wajibu wao kwa Taifa na watakaposhiriki Oparesheni za Ulinzi wa Amani.” Amesema Luteni Jenerali Salum Haji Othmani.  

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema Utafiti huo unafanyika nchini kwa mara ya kwanza na ni utafiti wa kwanza unafanywa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na JWTZ ambapo amesema NBS kama Mamlaka yenye dhamana ya kukusanya, kuchakata na kusambaza Takwimu, anaiona kuwa hiyo ni fursa ya ushirikiano kati ya NBS na JWTZ kama sehemu ya kupunguza pengo la takwimu lililopo katika masuala ya Ulinzi wa Amani.

Naye, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania – TPTC cha JWTZ ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Mradi huo, Brigedia Jenerali George Mwita Itang’are amesema mradi huo utatekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa awamu tano na yataangaliwa maeneo muhimu 10 yaliyoainishwa kimataifa.

Lengo kuu la Mradi huo ni kutathmini nafasi na vikwazo kwa Wanawake wa JWTZ kushiriki kikamilifu katika Operesheni za Ulinzi wa Amani ikiwa ni sehemu ya juhudi kubwa za Serikali za kuongeza viongozi wanawake katika kujenga na kudumisha amani ambapo matokeo yanayotarajiwa ni kuzalisha data na mapendekezo yatakayosaidia kuongeza idadi ya wanawake wanaopelekwa kwenye operesheni za ulinzi wa amani.