NBS Yaikabidhi NM – AIST Nakala Vitabu 228 vya Takwimu
Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS imeikabidhi Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela - NM-AIST nakala za vitabu 228 vya takwimu rasmi kwa lengo la kuimarisha ufundishaji, ujifunzaji na utafiti wa kisayansi katika taasisi hiyo.
Vitabu hivyo vinajumuisha machapisho mbalimbali yatolewayo na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikiwemo Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi, Takwimu za Ajira pamoja na taarifa nyingine muhimu za kijamii na kiuchumi. Machapisho hayo yanatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi, wahadhiri na watafiti wa NM-AIST katika shughuli zao za kitaaluma na kiutafiti.
Akizungumza wakati wa kupokea vitabu hivyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ubunifu wa NM-AIST, Profesa Anthony Mshandete, ameishukuru NBS kwa mchango huo muhimu, akibainisha kuwa vitabu hivyo vimewasilishwa kwa wakati muafaka.
Profesa Mshandete ameeleza kuwa vitabu hivyo vitakuwa msaada mkubwa hususan kwa wanafunzi walionufaika na Udhamini wa Masomo wa Samia uliopanuliwa katika fani za Sayansi ya Takwimu, Akili Unde (Artificial Intelligence) na Sayansi Shirikishi, waliojiunga na NM-AIST mwaka 2026 katika programu mpya ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Takwimu na Akili Unde (M.Sc. Data Science and Artificial Intelligence).
Aidha, ameongeza kuwa machapisho ya NBS pamoja na mifumo yake ya kidijitali, ikiwemo tovuti rasmi, yatawawezesha wanafunzi na watafiti kupata takwimu kwa urahisi zaidi. Hatua hiyo itachochea ubora wa utafiti, ubunifu na matumizi ya takwimu rasmi katika kuchangia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi nchini.