NBS Yashirikisha Wadau Maandalizi ya SP Mpya
Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS imefanya kikao na wadau wa Takwimu nchini wa sekta ya umma na sekta binafsi kwa lengo la kupokea maoni yao ili kuboresha rasimu ya Mpango Mkakati – SP wa Ofisi hiyo wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031 ambapo Mpango Mkakati wa Awali unafikia ukomo wake mwezi Juni 2026.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro uliopo kwenye Jengo la Makao Makuu ya Ofisi hiyo tarehe 11 Mei 2026 Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema Takwimu ni suala mtambuka na kwamba hakuna taasisi, idara, watafiti au sekta yoyte ile inayoweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo bila kuwa na Takwimu rasmi.
“Takwimu hizi mzalishaji wa kwanza ni wadau…lengo kubwa ni kuhakikisha mdau anapozalisha Takwimu ziwe na umuhimu, haziwezi kuwa na umuhimu kama hazitakuwa zimefuata viwango ambavyo vimewekwa kitaifa na kimataifa. Amesema Dkt. Msengwa na kuongeza;
“Ili kuzingatia hilo ndiyo maana tunaandaa Strategic Plan (Mpango Mkakati – SP), tunaiita ni Strategic Plan ya NBS lakini hii ni Strategic Plan ambayo itaongoza upatikanaji wa Takwimu nchini, maana yake ukitaka Takwimu zako ziweze kutumika kwa mapana yake lazima izingatie viwango na tunaamini kabisa itaweza ku-fit in (kufaa) kwenye hii Strategic Plan ambayo tunaizalisha.”
Kiongozi huyo amesema Mpango Mkakati huo ni nyenzo muhimu itakayoiwezesha Ofisi hiyo kuoanisha shughuli zake na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha takwimu zinakuwa na msingi sahihi katika kusaidia Serikali kupanga, kufuatilia na kutathmini hatua mbalimbali za maendeleo zinazofikiwa, pamoja na kubaini changamoto zinazowakabili Wananchi.
“Tunafahamu dunia la leo inaenda na sayansi, ukisema sayansi lazima uwe na evidence (ushahidi), kwa hiyo huu ushahidi wa kisayansi unatuambia sisi kama wazalishaji wa Takwimu, lazima tuzalishe Takwimu bora ambazo zitaleta tija na kuleta mipango itakayojibu matakwa ya Wananchi.” Amesema Dkt. Msengwa.
Ameongeza kwamba, kwa kuwa hilo ni takwa la msingi hivyo zinahitajika Takwimu za mara kwa mara (Real Time Data) ambapo Takwimu zinakusanywa katika muktadha ambao ni mpana kwa kuwa sekta ni nyingi na maeneo ni mengi, changamoto zinaibuka kila siku hivyo, kila zinapoibuka lazima zipatikane Takwimu zitakazosaidia.
Akizungumza awali Meneja wa Mipango na Bajeti Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Huzaima Kombe Mushi amesema rasimu hiyo tayari imeshapita katika hatua ya vikao mbalimbali na kupatiwa maoni ambapo alifafanua kuwa kikao hicho ni miongoni mwa hatua za mwisho ya kuwapitisha na kupata maoni ya wadau wa ndani na nje.
“Lengo la kikao hiki ni kuhakikisha wadau wote wanatoa maoni yao kwenye Mpango Mkakati wetu, ili uweze kuwa bora kwa sababu wao ndiyo watumiaji wakuu wa Takwimu rasmi nchini kwa sababu na wote ni member (wajumbe) wa NSS (Mfumo wa Taifa wa Takwimu).” Amesema Mushi.