The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS Yatoa Mafunzo kwa Wadadisi Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi Mwaka 2026
Posted On: 03 February, 2026
NBS Yatoa Mafunzo kwa Wadadisi Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi Mwaka 2026

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS imetoa mafunzo kwa Wadadisi 150 ambao watatumika kukusanya taarifa katika Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa Mwaka 2026, yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Mount Uluguru mkoani Morogoro kuanzia tarehe 26 Januari 2026 hadi 9 Februari 2026.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yenye lengo la kuwapatia Wadadisi hao mbinu na namna sahihi ya kukusanya taarifa za utafiti huo, Mtakwimu Mwandamizi Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Idara ya Ajira ambaye ni Afisa Dawati wa Utafiti huo, Hashim Njowele amesema kuwa utafiti huo unalenga kupata taarifa za soko la ajira nchini, ikiwemo idadi ya watu wenye ajira na idadi ya watu wasio na ajira.

Njowele ameeleza kuwa matokeo ya utafiti huo yatatumika kuunda na kutathmini sera mbalimbali zinazohusiana na soko la ajira, pamoja na mipango ya mafunzo na maendeleo ya rasilimali watu.

“Utafiti huu utafanyika nchi nzima kwa kutumia sampuli ya maeneo yaliyochaguliwa kitaalamu, ambayo yatatumika kuwakilisha maeneo mengine yote nchini.” Amesema Njowele na kuongeza;

“utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi hufanyika kila mwaka kwa awamu nne yaani kila robo ya mwaka, na kwa mwaka 2026, awamu ya kwanza ya utafiti itafanyika katika robo ya kwanza kuanzia Februari hadi Machi 2026.”

Njowele ametoa wito kwa Wananchi katika maeneo na kaya zitakazohusishwa katika utafiti huo kutoa ushirikiano kwa wadadisi, akisisitiza kuwa utafiti huo una manufaa makubwa kwa taifa katika kupanga na kutathmini sera za soko la ajira.

Aidha, ili kupata taarifa za uhakika na kwa ufanisi, mafunzo hayo yanajumuisha zoezi la ufanyaji wa mitihani kwa Wadadisi ili kupima uwezo wao, ambapo wale watakaofaulu ndiyo watakaoruhusiwa kuendelea na hatua ya ukusanyaji wa taarifa za utafiti huo, huku wasiofaulu wakibaki katika hatua ya awali ya mafunzo.