NBS Yatoa Wito kwa Wananchi Kutoa Ushirikiano wakati wa Utafiti wa Kilimo, Mifugo wa Mwaka 2024/2025
Na Sofia Charles, NBS
Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS imetoa wito kwa Wananchi nchini kutoa ushirikiano wakati wa wa zoezi la Utafiti wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa mwaka 2024/2025 ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazotumika kupanga maendeleo ya sekta hizo.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Utafiti wa Kilimo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Samuel Kawa, wakati wa mafunzo ya wiki mbili kwa Wadadisi na Wasimamizi wa Utafiti huo yanayoendelea kuanzia tarehe 24 Novemba hadi tarehe 0 Disemba 2025 kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Uluguru, mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kawa amesema takwimu zitakazokusanywa ni muhimu kwa Serikali na wadau kupanga mipango ya maendeleo ya kilimo, ufugaji na uvuvi nchini.
“Takwimu mtakazokusanya ndizo Serikali inazitumia kupanga bajeti, kutathmini uzalishaji pamoja na kutengeneza sera za kuinua kilimo. Ushirikiano wa Wananchi katika utafiti huu ni msingi wa kupata taarifa zinazoakisi hali halisi.” Amesema Kawa.
Kawa amefafanua kuwa utafiti huo utasaidia watafiti, wanafunzi na wananchi kupata taarifa za kitaalamu zitakazowezesha kutatua changamoto zilizopo katika kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kwa mujibu wa NBS, Utafiti wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa mwaka 2024/2025 unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 15 Desemba 2025, na utafanyika kwa miezi miwili katika maeneo yote nchini, ukihusisha kaya pamoja na mashamba makubwa.
Amesema utafiti huo utajikita katika kukusanya taarifa za uzalishaji wa mazao, matumizi ya pembejeo, idadi ya mifugo, matumizi ya teknolojia, na changamoto zinazowakabili wakulima na wafugaji.
“Lengo ni kupata takwimu za uzalishaji wa mazao, pembejeo na namna watu wanavyotumia njia tofauti za kilimo pamoja na matumizi ya pembejeo, na uelewa zaidi kwa mkulima ili Serikali na wadau waweze kupanga mikakati ya kuboresha uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji.” Amesema Kawa.
NBS imewahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakapofika kwenye kaya zao ili kufanikisha upatikanaji wa takwimu sahihi na zenye uhalisia.