SG Dkt. Msengwa Afanya Mazungumzo, Ujumbe Kutoka UNICEF
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto – UNICEF, makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma tarehe 19 Januari 2026.
Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha na kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya ofisi hizo hususan katika uzalishaji wa takwimu za kijamii.
Dkt. Msengwa amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo ya takwimu nchini kupitia utekelezaji wa Mfumo Jumuishi wa Takwimu - TISP pamoja na maboresho ya tafiti za kitaifa, hatua inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa takwimu bora, kwa wakati na zinazotumika moja kwa moja katika kupanga sera na mipango ya maendeleo.
Kiongozi huyo amesema Mfumo huo ambao umezinduliwa tarehe 18 Novemba 2025, umeanza kuonesha matokeo chanya kwa kuunganisha data kutoka sekta mbalimbali za Serikali, licha ya changamoto za awali zilizotokana na tofauti ya mifumo na miundombinu ya takwimu.
Ameeleza kuwa kwa sasa changamoto hizo zinaendelea kushughulikiwa, huku taratibu za ujumuishaji wa mifumo zikiboreshwa ili kurahisisha mtiririko wa takwimu ambapo amesema lengo la Serikali ni kuongeza idadi ya sekta zilizounganishwa katika Mfumo wa TISP hadi kufikia zaidi ya sekta 28 ifikapo mwaka 2027.
Dkt. Msengwa amebainisha kuwa pamoja na kuwepo kwa Mfumo wa TISP, maandalizi ya tafiti mbalimbali za kitaifa yanaendelea, ikiwemo Utafiti wa Kutathmini Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira – WASH wa Mwaka 2025, Utafiti wa Nguvu Kazi - ILFS, Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto - DHS pamoja na Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi - IHBS.
Pia, amebainisha kuwa Serikali inalenga kuanza mapema uchambuzi wa takwimu badala ya kusubiri kukamilika kwa ukusanyaji wote, hatua itakayopunguza muda wa utoaji wa taarifa na kusaidia watunga sera kupata vielelezo muhimu kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Msengwa amesema NBS ina mpango wa kuanzisha Kituo cha Kuchakata na Kuchambua Data kwa Kina (Data Analytic Hub) kitakachotumia teknolojia bunifu na mifumo ya kiotomatiki kuzalisha taarifa za mara kwa mara, ikiwemo za kila mwezi au robo mwaka.
“Lengo letu ni kuhakikisha takwimu zinaanza kutumika mapema katika kupanga mipango ya maendeleo na si kusubiri ripoti baada ya miezi kadhaa.” Amesema Dkt. Amina Msengwa.
Dkt. Msengwa amewashukuru Viongozi hao wa UNICEF Tanzania na wadau wengine kwa kuendelea kutoa msaada wa kiufundi, kuwajengea uwezo Watakwimu na kuunga mkono mageuzi ya mifumo ya takwimu nchini.
Alisema ushirikiano huo umechangia mafanikio katika tafiti za umaskini wa watoto, uchambuzi wa faida ya idadi ya watu na mijadala ya umma inayotumia takwimu kama msingi wa sera.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sera za Kijamii wa UNICEF Tanzania, Diego Angemi amesema Shirika hilo litaendelea kuunga mkono ajenda za Serikali kwa kuhakikisha takwimu zinazokusanywa zinatumika kikamilifu katika kuboresha maisha ya Wananchi hususan watoto na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.
Pamoja na hayo, Dkt. Msengwa amemkabidhi mwakilishi huyo wa UNICEF nakala tatu kati ya nane za ripoti za kina zitokanazo na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, zilizozinduliwa Mwezi Novemba 2025 ambazo ni Ripoti ya Elimu na Hali ya Kujua Kusoma na Kuandika Tanzania, Ripoti ya Hali ya Uzazi na Vifo Tanzania na Ripoti ya Hali ya Uchambuzi wa Vifo Tanzania.