SG Dkt. Msengwa Afunga Warsha ya Kitaifa Upatikanaji Takwimu za Kupima Mabadiliko ya Tabianchi
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa leo tarehe 02 Septemba 2026 amefunga warsha ya kitaifa ya siku mbili kuhusu upatikanaji wa Takwimu za kupima mabadiliko ya Tabianchi nchini, kwa mtazamo wa kijinsia kwa ajili ya kuboresha sera za kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Akizungumza wakati wa hotuba ya kufunga warsha hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Serengeti uliopo katika Hoteli ya Best Western Dodoma City jijini Dodoma, Dkt. Msengwa amesema Tanzania inajivunia kuwa miongoni mwa nchi tano za majaribio zilizoteuliwa kutekeleza Mradi wa Akaunti ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa chini ya Awamu ya 17, unaolenga eneo hilo muhimu.
Dkt. Msengwa ametumia nafasi hiyo kulishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira - UNEP na Divisheni ya Takwimu ya Umoja huo - UNSD kwa ushirikiano wao endelevu kwa Tanzania ambapo amesema Tanzania inaliona hilo kuwa ni fursa kubwa ya kuboresha sera zake za kitaifa kuhusu tabianchi na jinsia, pamoja na kushirikisha uzoefu wake katika kuendeleza mbinu na mifumo ya kitakwimu yenye manufaa ambayo inaweza kutumika pia katika ngazi za kikanda na kimataifa.
Kiongozi huyo amesema warsha hiyo imedhihirisha kwa uwazi umuhimu wa kuwa na takwimu rasmi zenye ubora wa juu zinazobainisha kwa kina vipengele vya kijinsia vinavyohusiana na mabadiliko ya tabianchi, ambazo ni muhimu katika kubuni sera zinazozingatia namna tofauti ya wanawake na wanaume wanavyokabiliwa na hatari za mabadiliko hayo pamoja na kufuatilia maendeleo kwa usawa zaidi.
“Takwimu za tabianchi hazipaswi kuishia katika wastani wa kitaifa pekee bali zinapaswa kutueleza nani anaathirika, anaathirika wapi, anaathirika kwa namna gani, na kwa nini athari za mabadiliko ya tabianchi zinatofautiana kati ya jamii na makundi mbalimbali ya watu.” Amesema Dkt. Msengwa na kuongeza;
“Tunapoendelea na utekelezaji wa Dira 2050 pamoja na vipaumbele vyetu vya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ni muhimu kuendelea kuziba pengo kati ya takwimu na sera.”
Dkt. Msengwa amefafanua kuwa Takwimu zinapaswa kuwa msingi wa kufanya maamuzi, kugawa rasilimali, kubuni programu na kufuatilia utekelezaji na matokeo.
Ikumbukwe kuwa orodha ya Kimataifa ya Takwimu na Viashiria vya Mabadiliko ya Tabianchi, mahitaji ya utoaji wa taarifa chini ya Mkataba wa Paris wa Mwaka 2015, matokeo ya Utafiti wa Jinsia na Mazingira Tanzania wa Mwaka 2025, pamoja na vipaumbele na vyanzo vingine vya takwimu za kitaifa vinaimarisha upatikanaji wa ushahidi wa kitakwimu unaohitajika katika utungaji wa sera, upangaji wa mipango, ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa.
Washiriki wa warsha hiyo ni wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Madini na Wizara ya Maji.
Wataalam wengine wanaoshiriki warsha hiyo ni kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Afya, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Tume ya Mipango, Mamlaka ya Hali ya Hewa - TMA, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira - NEMC, Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni – NCMC, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - UDSM, Chuo Kikuu cha Dodoma – UDOM, Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC na Mtandao wa Jinsia Tanzania – TGNP.