SG Dkt. Msengwa Akutana, Wataalam wa ONS
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS Tanzania, Dkt. Amina Msengwa amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Uingereza - ONS-UK ikiwa ni sehemu ya kudumisha ushirikiano baina ya ofisi hizo mbili.
Mazungumzo hayo ambayo yamefanyika ofisini kwake Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma tarehe 26 Januari 2026 yamelenga kubadilishana na kupeana ujuzi juu ya matumizi ya teknolojia za kisasa katika ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu (Big data).
Pia, maeneo mengine yaliyojadiliwa ni kuona namna bora na thabiti ya kujilinda na mashambulio ya kimtandao pamoja na uimarishaji wa mifumo ya Takwimu za Kiutawala.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Emily Posket na Garnett Compton ambao ndiyo wawakilishi wa ONS-UK wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kujenga mfumo imara wa Takwimu nchini.
Pia, Waatalam hao wamepata muda wa kujadiliana na Wataalam wa TEHAMA wa NBS kuhusu namna ya kutumia Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) katika usalama wa Mifumo ya TEHAMA.
Aidha, SG Dkt. Msengwa aliwaongoza wageni hao kutembelea Kituo cha Mawasiliano (Call Centre) cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambapo walijionea programu inayotumika kurekodi mahojiano wakati wa tafiti mbalimbali zinazofanyika kwa njia ya simu.