SG DKT. Msengwa Aongoza Kikao cha Wadau Kujadili Itifaki ya SADC Ihusuyo Masuala ya Takwimu
SG DKT. Msengwa Aongoza Kikao cha Wadau Kujadili Itifaki ya SADC Ihusuyo Masuala ya Takwimu
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa ameongoza kikao kazi cha wadau kujadili Itifaki ya Takwimu ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC (SADC Protocol on Statistics) kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro uliopo katika Jengo la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma tarehe 20 Januari 2026 kikiwa na lengo la kupitia na kupokea maoni ya Itifaki hiyo juu ya masuala ya Takwimu.
Akifungua kikao hicho, Dkt. Msengwa amesisitiza kupitia na kupata maboresho ili kuweza kuipeleka mbele Itifaki hiyo na kuhakikisha mariadhiano kwa ajili ya matumizi ya nchi kwa lengo thabiti la kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa takwimu.
“Sisi kwetu hii tunaichukua kama fursa na faida kubwa ambayo inaweza kuonekana ni pamoja na kujengewa uwezo wa kitaalamu kwa watakwimu lakini pia na kada ambazo zinaendana na utakwimu tukimaanisha kwamba tutaweza sasa kuendelea kufanya tathmini tukizingatia tuna takwimu bora na zinazopatikana kwa wakati.” Amesema Dkt. Msengwa na Kuongeza;
“Tutaweza kuimarisha ulinganifu wa takwimu zetu, kati ya nchi yetu nan chi wanachama…kwa mantiki hiyo sasa tunaona Takwimu zetu zinaweza kuchochea uwekezaji, ajira na mapato ya Serikali na ukuaji wa uchumi. Hivyo, tuichukue Itifaki hii kwamba ni msingi wa kuhakikisha mfumo wetu wa takwimu ni imara na ni bora na tunaweza kupata takwimu ambazo zitakidhi matakwa ya nchi na matakwa ya nchi shirikishi.”
Akizungumza awali, Mkuu wa Kitengo cha Sheria Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Oscar Mangula amesema katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali Wanachama wa SADC uliofanyika Lilongwe, Malawi mwaka 2021, Sekretarieti ya SADC iliwasilisha Itifaki ya Takwimu kwa Nchi Wanachama ambayo ilikubaliwa na Wakuu hao. Kufuatia hatua hiyo, Nchi wanachama ziliaanza mchakato wa kusaini na kuiridhia Itifaki hiyo ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini Itifaki hiyo tarehe 18 Agosti 2021.
Mangula ameongeza kuwa lengo la Itifaki hii ni kutoa mwongozo kuhusu umuhimu wa takwimu katika kufuatilia maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kupunguza umaskini na kuweka mazingira wezeshi ya ukuaji wa uchumi kwa kuzingatia uwianishaji na kuweka pamoja rasilimali kwa njia ya kujitegemea ili kuboresha hali ya maisha ndani ya Jumuiya.
Amesema lengo la pili ni kuwa na Mfumo bora wa kuratibu upatikanaji na usambazaji wa takwimu za kiuchumi na kijamii zitakazotumika katika kupanga na kutolea maamuzi mbalimbali ya kisera katika ngazi ya Taifa na Jumuiya.
Baadhi ya wadau walitoa maoni mbalimbali juu ya maboresho ya Itifaki ya SADC katika masuala ya Takwimu huku wakisisitiza juu ya umuhimu wa matumizi na usambazaji wa takwimu sahihi ili kuweza kuleta tija katika maendeleo ya nchi kiujumla katika kutunga sera na kuanzisha miradi mbalimbali kwa kutumia takwimu sahihi.
Mangula amesema faida ambazo Tanzania itazipata kwa kuridhia Itifaki ya Takwimu ni pamoja na kutumia fursa zinazoratibiwa na SADC katika kujenga uwezo wa watakwimu nchini, kwa ajili ya kuboresha uzalishaji wa takwimu rasmi zitakazohitajika katika kufuatilia na kutathmini viashiria vilivyoainishwa katika Dira ya SADC 2050, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050), Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050, Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Dunia (Sustainable Development Goals - SDG’s) ya mwaka 2030 na Agenda ya Afrika ya Mwaka 2063 kwa kutumia ushirikiano uliopo miongoni mwa nchi wananchama wa SADC.
Wadau waliodhuria kikao hicho ni kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Fedha, Wizara ya Uchukuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (OWM – TAMISEMI), Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Maji, Mamlaka ya Serikali Mtandao pamoja na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.