The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
SG Dkt. Msengwa Awaongoza Wadau Kuhakiki Ripoti ya Kina ya Uhamaji na Ukuaji wa Miji
Posted On: 15 December, 2025
SG Dkt. Msengwa Awaongoza Wadau Kuhakiki Ripoti ya Kina ya Uhamaji na Ukuaji wa Miji

Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS imewasilisha kwa wadau Ripoti ya Kina  itokanayo na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kuhusu Uhamaji na Ukuaji wa Miji, katika kikao cha uwasilishaji wa Ripoti hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano uliopo ofisi ndogo za NBS Kivukoni jijini Dar es Salaam leo tarehe 12 Disemba 2025.

Akifungua kikao hicho Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema Ofisi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa taarifa zinazokusanywa hazibaki ndani ya mikono ya NBS bali ziwe chachu na muendelezo wa kuhakikisha kuwa zinaendelea kutumika katika kufanya tathmini kwa kuzingatia takwimu rasmi zinazozalishwa.

Akizungumza awali Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022, Phausta Ntigiti ameeleza kuwa, kufanyika kwa kikao hicho ni hatua muhimu ya maandalizi ya ripoti za kitakwimu katika kuhakikisha kuwa uchambuzi uliofanyika unakidhi vigezo vya ubora vya ndani na vya Umoja wa Mataifa (UN Fundamental Principles of Official Statistics). Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ripoti hiyo inaakisi hali halisi ya mahitaji ya takwimu kwa ajili ya kuwezesha kupanga, kupima na kutathmini hali ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya ndani, kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake Mtaalamu Mshauri, Dkt.  Rutasha Dadi amesema sensa inaongoza kwa utajiri wa taarifa na kuwa ni chanzo kikubwa cha takwimu kwa ajili ya mipango na sera kwa mamlaka husika ambapo unaweza kupata taarifa hadi ngazi ya chini ya jamii. 

Aidha, akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya Uhamaji nchini - IOM, Maurizio Bussati  amewashukuru washiriki na waandaaji wa Ripoti hiyo ambapo ameomba kufanyia kazi na kukamilisha maboresho yaliyotolewa na wadau. 

Aidha, Busatti amewashukuru viongozi wa NBS na Serikali kwa ujumla, kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata hususan katika kuwezesha upatikana wa Takwimu sahihi kwa matumizi ya mipango mbalimbali ambayo ndiyo inayowezesha mipango ya maendeleo.