The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
SG Dkt. Msengwa Awapongeza, Kuwashukuru Wananchi kwa Ushirikiano kuhusu Utafiti wa Kilimo Unaoendelea nchini
Posted On: 09 January, 2026
SG Dkt. Msengwa Awapongeza, Kuwashukuru Wananchi kwa Ushirikiano kuhusu Utafiti wa Kilimo Unaoendelea nchini

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amewapongeza na kuwashukuru Wananchi kwa namna wanavyotoa ushirikiano wa uoaji wa taarifa kwa Wadadisi katika Utafiti wa Kilimo wa Mwaka 2024/2025 unaoendelea nchini.

Dkt. Msengwa ametoa pongezi na shukrani hizo alipotembelea uwandani kwenye baadhi ya Kaya katika Kata za Mwakibete na Uyole zilizopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya mkoani Mbeya tarehe 07 Januari 2026.

Kiongozi huyo ametembelea uwandani kujionea maendeleo ya zoezi la utafiti huo unaofanyika kwa kipindi cha miezi miwili (Januari hadi Februari 2026), ukiwa na lengo la kukusanya takwimu kuhusu ukubwa wa maeneo ya kilimo na uzalishaji wa mazao, idadi ya mifugo na mazao yatokanayo na mifugo pamoja na ufugaji wa viumbe maji.   

Akiwa uwandani Dkt. Msengwa amewasisitiza Wadadisi kufanya kazi hiyo kwa weledi kwa kuzingatia maelekezo na mafunzo waliyopatiwa na Ofisi hiyo siku chache kabla ya kuanza kwa zoezi hilo na kwamba matokeo yatakayotokana na taarifa wanazozikusanya yana tija kwa taifa kwa ajili ya kupanga mipango ya kuwaletea maendeleo Wananchi.

SG Dkt. Msengwa kabla ya kwenda uwandani amemtembelea ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Moris Malisa ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao wametumia nafasi hiyo kufanya mazungumzo yenye lengo la kudumisha ushirikiano baina ya ofisi hizo ili kuwaletea Wananchi maendeleo.

Pia, Mtakwimu Mkuu wa Serikali alitembelea Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Mbeya iliyopo Mtaa wa Block T Kata ya Iyela, ambapo amekutana na kuzungumza na Watumishi wa ofisi hiyo, ambapo amewataka kuendelea kufanya kazi kwa bididii na kwa weledi kwa kudumisha ushirikiano baina ya Ofisi hiyo na taasisi nyingine za Serikali na Wadau mbalimbali.