The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
SG Dkt. Msengwa wakaribisha Watumishi Wapya NBS
Posted On: 12 February, 2026
SG Dkt. Msengwa wakaribisha Watumishi Wapya NBS

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amewakaribisha rasmi Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS Watumishi ajira mpya 21 ambao wameajiriwa ndani ya Siku 100 za uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Sita Kipindi cha Pili, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro uliopo kwenye jengo la makao makuu ya Ofisi hiyo jijini Dodoma tarehe 09 Februari 2026. 

Dkt. Msengwa, amewasisitiza watumishi hao kuzingatia Sheria ya Takwimu Sura ya 351, miongozo ya kitaaluma ya takwimu pamoja na taratibu za taasisi kwa kuwa takwimu ni msingi muhimu katika upangaji wa mipango na maamuzi ya Serikali, hivyo ni wajibu wao kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.

Aidha, Dkt. Msengwa amewakumbusha watakwimu hao kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya taaluma kwa weledi, uhuru na kuhakikisha usiri wakati wa uchakataji wa taarifa mbalimbali. 

Pia, amewaeleza kuwa wanapaswa kuzingatia maadili na utamaduni wa taasisi katika utendaji wao wa kila siku huku wakiwa tayari kujifunza na kujiendeleza kitaaluma kwa manufaa ya taasisi na taifa kwa ujumla.

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uelewa wa mwelekeo wa utendaji wa kazi na majukumu yao pamoja na kufahamu taratibu, ushirikiano wa idara na utamaduni wa taasisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Pamoja na mambo mengine, Wajumbe wa Timu ya Menejimenti ya NBS wamepata nafasi kielezea majukumu na shughuli mbali zinazotekelezwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupitia idara mbalimbali.