The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Wadadisi Waandaliwa Kukusanya Taarifa Utafiti wa WASH - HCFs 2025/2026
Posted On: 12 February, 2026
Wadadisi Waandaliwa Kukusanya Taarifa Utafiti wa WASH - HCFs 2025/2026

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar - OCGS, inaendesha mafunzo kwa Wadadisi na Wasimamizi kwa ajili ya kukusanya taarifa za Utafiti wa Kutathmini Upatikanaji wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika Vituo vya Kutolea Huduma za Afya – WASH - HCFs wa Mwaka 2025/2026.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Arusha tarehe 09 Februari 2026, Kaimu Meneja wa Takwimu za Jamii na Demografia, Elinzuu Nicodemo Yohana, amesema Wadadisi hao wanatakiwa kuwa makini kufuatilia mafunzo ya nadharia na vitendo kwa kuwa ndiyo msingi wa kupata Takwimu Bora.

“Niwasihi Wadadisi mfuatilie kwa umakini mafunzo haya mnayopewa ili muweze kukusanya taarifa zenye ubora kwa kuwa huo ndiyo msingi wa kupata Takwimu zenye viwango stahiki.” Amesema Yohana katika mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 09 hadi 14 Februari 2026.

Akitoa maelezo ya utekelezaji wa utafiti huo, Mtakwimu Mwandamizi ambaye pia ni Afisa Dawati wa WASH - HCFs 2025, Prisca Mkongwe amesema utafiti huo unatekelezwa nchi nzima ukihusisha mikoa 26 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar.ikoa mitano ya Zanzibar.

Prisca amesema Wadadisi 30 watakusanya taarifa katika vituo vya kutolea huduma za afya 514 vilivochaguliwa, kwa lengo la kutathmini huduma zinazopatikana katika Vituo hivyo hususan vyoo, maji, na usafi wa mazingira kwa ujumla.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM – TAMISEMI), Wizara ya Maji, Vyuo Vikuu vya Mzumbe, Dodoma, Dar es Salaam pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto - UNICEF ambalo ndilo linalofadhili utafiti huo.

“Lengo ya utafiti huu ni kutathmini huduma za vyoo, maji na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo niwaombe wakati wa kukusanya taarifa mtatakiwa kujituma na kufanya kazi kwa uadilifu ili kupata takwimu bora zitakazoisaidia Serikali kutunga sera na kupanga mipango ya maendeleo nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Takwimu za Kijamii, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Fahima Mohamed Issa, amewasisitiza Wadadisi kuwa makini wakati wa kukusanya taarifa kwani kinyume na hivyo basi takwimu zitakazopatikana haziwezi kuwa sahihi kwa kuwa taarifa hzo ndiyo muhimili wa Takwimu bora.

“Msipoelewa ulizeni ili muelekezwe, fuateni maelekezo ya walimu wenu na fanyeni kazi kwa ushirikiano. Pia, niwaombe Wasimamizi wasimamieni ili taarifa zitakazochukuliwa ziwe sahihi.” Amesema Issa.