The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Wataalam NBS, OCGS, UDSM Wajengewa Uwezo Uchambuzi wa Sampuli
Posted On: 01 March, 2026
Wataalam NBS, OCGS, UDSM Wajengewa Uwezo Uchambuzi wa Sampuli

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika - SADC imeratibu mafunzo maalum ya mbinu za uandaaji na uchambuzi wa sampuli za tafiti kwa wataalamu wa takwimu kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kitaalamu katika taasisi za takwimu nchini.

Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia tarehe 23 hadi 27 Februari 2026 katika Ukumbi wa Midland Hotel jijini Dodoma, yakihusisha washiriki 19 wa NBS, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar - OCGS, pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - UDSM.

Akifunga mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu, Tafiti na Operesheni za Kitakwimu, James Mbogo amewahukuru wawezeshaji kutoka SADC kwa mchango wao katika kuwajengea uwezo washiriki.

Mbongo amesema NBS itaendelea kutafuta na kutumia fursa mbalimbali za kimasomo na kujengeana uwezo ili kuimarisha uwezo wa kitaalam na kuboresha utendaji kazi.

Naye, Mtakwimu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Lathma Iddy amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki katika kubuni, kuandaa na kusimamia mbinu za utayarishaji Sampuli za Takwimu pamoja na kuwapatia mafunzo ya vitendo kwa kutumia programu za uchambuzi kama vile R.

Aidha, Iddy amesema kuwa matarajio ya mafunzo hayo kwa washiriki ni kuelewa dhana za msingi za ubunifu na uandaaji wa sampuli katika tafiti za kitakwimu, pamoja na hatua mbalimbali zinazohusika katika mchakato huo, ambapo pia amesema yatawajengea washirki uwezo wa kutumia mbinu tofauti za kuchagua sampuli za uwakilishi.

Kadhalika, Mafunzo hayo yametolewa ili kuwajengea uwezo wa wakufanya mahesabu ya ukubwa wa sampuli, marekebisho ya kutokujibu (non-resonse adjustment) pamoja na makadirio ya tofauti,katika tafiti za takwimu.

Aidha, Iddy ametoa wito kwa washiriki kuhakikisha kuwa wanaendeleza  maarifa na ujuzi walioupata kwa kujisomea zaidi na kuyatimiza ipasavyo katika majukumu yao ya kila siku, amesisitiza kuwa hatua hiyo itachangia kuongeza idadi ya wataalamu wenye umahiri katika eneo la uandaaji wa sampuli na kuboresha ubora wa takwimu rasmi zinazozalishwa nchini.