The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Wataalam NBS, OCGS, UDSM Wapatiwa Mafunzo ya Programu ya Uchambuzi wa Takwimu
Posted On: 22 January, 2026
Wataalam NBS, OCGS, UDSM Wapatiwa Mafunzo ya Programu ya Uchambuzi wa Takwimu

Wataalamu wa Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar – OCGS na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – UDSM wanashiriki mafunzo ya Programu ya Uchambuzi wa Takwimu ijulikanayo kama R and Power BI yanayofanyika kwa siku 12 kuanzia tarehe 19 hadi 30 Januari 2026, kwenye Ukumbi wa Four Points jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yanayotolewa na kufadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji – IOM yana lengo la kuwajengea uwezo zaidi wataalamu wa kuchambua taarifa mbalimbali hasa zinazotokana na Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi.

Akizungumza wakati wa kuanza mafunzo hayo Mtakwimu Mkuu Idara ya Sensa na Matukio Muhimu ya Binadamu – NBS, Phausta Ntigiti amesema mafunzo hayo yana lengo la kuimarisha uwezo wa uchambuzi na uwasilishaji wa takwimu katika usimamizi wa taarifa za uhamiaji.

Aidha, Ntigiti ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha watakwimu hao kuweza kuchambua taarifa kutoka kwenye Sensa na tafiti mbalimbali, kuwawezesha kuandaa Habari Picha (Infographics) kwa ajili ya kuchapisha na kusambaza matokeo ya sensa na tafiti hizo ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa kitaifa wa takwimu za uhamiaji.

Mafunzo hayo yanawashirikisha watakwimu 10 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, 10 kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar na wanne kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.