Watakwimu NBS Wapatiwa Mafunzo Matumizi Mfumo wa Takwimu za Pato la Taifa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS imefanya kikao kazi pamoja na mafunzo kwa watakwimu wa Idara ya Takwimu za Pato la Taifa kuhusu Mfumo wa Kuhifadhi, Kuchambua na Kukokotoa Takwimu za Pato la Taifa – NADABAS yanayofanyika Ofisi za NBS zilizopo Kivukoni jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 05 hadi 24 Januari 2026.
Akizungumza katika kikao kazi hicho Mtakwimu Mkuu Idara ya Takwimu za Pato la Taifa, Edith Sulla amesema mfumo huo unatekelezwa ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kukidhi matakwa ya makubaliano ya Jumuiya za kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Afika Mashariki – EAC, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC na Umoja wa Afrika – AU katika eneo la maendeleo ya Takwimu.
Mtaalam huyo ameeleza kuwa mfumo huo unalenga kurahisisha uhifadhi wa Takwimu, kusaidia ulinganifu wa Takwimu za Pato la Taifa na nchi nyingine wanachama.
Kikao hicho ni juhudi endelevu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kuboresha mfumo wa takwimu na kurahisisha matumizi sahihi ya takwimu katika kupanga na kutekeleza sera mbalimbali katika kufikia malengo ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa.