Waziri Dkt. Gwajima Azindua Matokeo ya Tafiti Mbili
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima tarehe 06 Mei 2026 amezindua rasmi matokeo ya tafiti mbili ambazo ni Uwezeshwaji wa Wanawake na Lishe - WEN Msimu wa Kilimo 2023/2024 pamoja na Jinsia na Mazingira wa mwaka 2025 – TGES zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS.
Akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Ngorongoro Jengo la Makao Makuu ya NBS, Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa ipo haja ya kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto za usawa wa kijinsia, lishe na mazingira.
Mhe. Dkt. Gwajima amesema tafiti hizo zinaonesha kuwa, ni asilimia 26 tu ya wanawake ndiyo wanaamini wana uhuru wa kufanya maamuzi ya kiuchumi, huku asilimia 34.1 wakikubali kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu ndoa, talaka na uzazi na asilimia 54.6 wakikataa aina zote za ukatili wa kijinsia.
Aidha, amesema bado kuna pengo kubwa katika maamuzi ya kifedha, ambapo wanaume wanaongoza kwa asilimia 54.8 dhidi ya wanawake ambao ni asilimia 39.6. Hata hivyo, Dkt. Gwajima amesema wanawake wana ushawishi mkubwa zaidi katika matumizi ya muda kwa asilimia 43.3 ikilinganishwa na wanaume ambao wao ni asilimia 39.4.
Katika eneo la rasilimali na lishe, Kiongozi huyo amesema asilimia 58 ya wanawake wanatumia huduma za kifedha ikilinganishwa na asilimia 72 ya wanaume, huku asilimia 40 wakimiliki mali, lakini wachache wakiwa na umiliki rasmi.
Kwa upande wa lishe, Dkt. Gwajima amesema asilimia 56.7 ya wanawake wanakidhi kiwango cha chini cha lishe bora, huku baadhi ya maeneo ya vijijini yakishuka hadi asilimia 39 kutokana na upatikanaji mdogo wa vyakula muhimu.
Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwezeshwaji wa wanawake kupitia upatikanaji wa mikopo, elimu ya kifedha na umiliki wa mali, pamoja na kuongeza ushiriki wao katika maamuzi na nafasi za uongozi. Aidha, juhudi zitaelekezwa katika kuhamasisha lishe bora, kuimarisha matumizi ya takwimu katika mipango ya maendeleo, na kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika masuala ya mazingira ili kujenga jamii yenye ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.