The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Community should Eliminate the Notion that Statistics are only for Government Use
Posted On: 21 November, 2025
Community should Eliminate the Notion that Statistics are only for Government Use

Jamii pamoja na wadau wote nchini wametakiwa kuondoa dhana iliyojengeka kuwa Takwimu ni kwa ajili ya matumizi ya Serikali pekee.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu Eli-maamry Mwamba ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma tarehe 18 Novemba 2025.

Katika kusherehekea Siku hiyo ambayo huadhimishwa tarehe 18 Novemba kila mwaka, Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS imezindua rasmi Ripoti za Makadirio ya Idadi ya Watu katika ngazi ya Halmashauri kwa mwaka 2023 – 2050 katika Halmashauri 195 za Tanzania Bara na Zanzibar, Mfumo Jumuishi wa Takwimu Tanzania - TISP na Shindano la Ubunifu katika Takwimu (Data Challenge).

“Tunapoadhimisha siku hii ya leo, wajibu wetu mkubwa ni kukumbushana na kusisitiza zaidi, umuhimu wa Takwimu na matumizi yake katika ngazi zote za utawala, kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi ya chini kabisa, natoa rai kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na Wananchi kwa ujumla kuondoa dhana iliyojengeka kwa baadhi yetu katika jamii kuwa takwimu ni kwa ajili ya matumizi ya Serikali pekee.” Amesema Mwandumbya na kuongeza;

 

“Nimefurahi kusikia kuwa kabla ya Sikuhii ya kilele cha maadhimisho, kumekuwa na mfululizo wa matukio mbalimbali ikiwemo maonesho ya huduma na bidhaa zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mafunzo kuhusu uzalishaji na matumizi ya Takwimu, pia mada mbalimbali zimeendelea kuwasilishwa.”

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema kufanyika kwa maadhimisho hayo, kunasogeza masuala ya tasnia ya Takwimu karibu na Wananchi ili nao waweze kuona uhusiano kati ya Takwimu na maendeleo ya nchi yetu kijamii, kiuchumi na kisiasa na kwa kwamba sehemu kubwa ya takwimu inazalishwa katika ngazi ya kaya kupitia tafiti mbalimbali na sensa.

Amesema takwimu ni muhimu katika kutambua na kubainisha mahitaji ya Wananchi, kuweka malengo, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wake kwakuwa Takwimu zinazozalishwa zinatumia kodi za Wananchi hivyo, ni lazima zikidhi mahitaji ya Serikali kwa kusaidia kuleta ufanisi wa shughuli zake za msingi na kutoa muelekeo wa muda mrefu wa sera za nchi.

Kadhalika, amesema Takwimu hizo ziwawezeshe Wananchi na wadau wengine kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Serikali na mabadiliko yanayotokea katika kuimarisha ustawi wao ambapo alifafanua kuwa kwa lugha rahisi Takwimu ziwasaidie Wananchi kupima uwajibikaji wa Serikali yao, zikidhi mahitaji ya watumiaji na ziweze kujibu maswali kutoka kwa watunga sera na wafanya maamuzi.

Pia, amesema Mfumo Jumuishi wa Takwimu Tanzania - TISP ni jukwaa litakalowawezesha watumiaji kufanya uchambuzi mpana na mtambuka wa takwimu kwa kuunganisha viashiria kutoka mifumo yenye taarifa za kiutawala, kisekta, kidemografia na tafiti. Mfumo huo unarahisisha upatikanaji wa takwimu katika kituo kimoja, unaongeza uwazi na ubora wa taarifa na kuimarisha matumizi ya takwimu katika kupanga kutekeleza, kufatilia na kufanya maamuzi ya kibajeti yenye tija.

Aidha, ameipongeza menejimenti ya NBS kwa usimamizi wake bora na makini wa shughuli za kitakwimu chini ya uongozi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali na watumishi wa NBS kwa kujituma kwa juhudi na maarifa na washirika wa ndani na nje ambao wamekua wakishirikiana na NBS katika kuboresha shughuli za takwimu.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Takwimu utawezesha mifumo mbalimbali kusomana, kurahisisha utapitakanaji wa taarifa za kitakwimu na kuwezesha NBS  kutoa takwimu kwa wiki au kwa mwezi. Aidha, amewashukuru Wananchi wote kwa ushirikiano kwani takwimu hizo zinatoka kwao na amewaomba kuendelea kuwa tayari pale wadadisi wanapowafikia, kutoa majibu ambayo ni sahihi ili kuzalisha takwimu bora kwa maendeleo ya taifa ambapo amesema ofisi hiyo itaendelea kushirikisha wadau wengi zaidi katika kuhakikisha kuwa inazalisha Takwimu na zinaifikia jamii.

Kwa niaba ya wadau wa maendeleo UNFPA,UNICEF na EAC, Mwakilishi kutoka UNICEF  Mlemba Abassy Kamwe wameishukuru NBS kwa hatua hiyo kwani wanatambua umuhimu wa takwimu katika kupanga sera bora, ugawaji wa rasilimali, kufanya uwekezaji na kuboresha huduma za kijamii. Hivyo, Wadau hao wataendelea kutekeleza wajibu wao kikamilifu na kuimarisha ushirikiano  na NBS na wadau wengine muhimu katika kuboresha mifumo ya kitakwimu katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Na kuwa uzinduzi wa mfumo jumuishi wa takwimu Tanzania  unaonesha uwajibikaji na utayari wa serikali ya Tanzania katika kuboresha miundombinu yake ya kitakwimu, kuwekeza katika kujenga uwezo wa kitakwimu na kukuza ubunifu ili kuendana na kanuni za kimataifa za takwimu rasmi na maendeleo endelevu kwa kila mtu.

Naye, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda amesema kuwa takwimu ni msingi wa maamuzi sahihi, sera zenye ushahidi na mipango endelevu ya kijamii na kiuchumi. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya takwimu katika ngazi zote za maamuzi kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, Halmashauri, familia, jamii, hadi taifa.

Maadhimisho hayo ambayo yalianza rasmi mwaka 1990 barani Afrika, kwa mwaka 2025 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo;  ‘’Kuongeza ubunifu katika matumizi ya Takwimu na Taarifa ili kujenga Jamii Jumuishi inayojali Haki,Amani na Maeneleo kwa Waafrika.”