Karibu
Taarifa kutoka kwa Mtakwimu Mkuu
Nikiwa Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nina furaha kuongoza juhudi za taifa letu katika kutoa takwimu rasmi zenye ubora wa hali ya juu, kwa wakati na zinazotegemewa ili kusaidia maamuzi yanayozingatia ushahidi wa kitakwimu na maendeleo ya kitaifa. NBS ina jukumu muhimu katika Ajenda ya Maendeleo ya Tanzania kwa:
a. Kukusanya, kuchambua, na kusambaza takwimu za kiuchumi, kijamii, kidemografia na mazingira kwa kina kuhusu nchi yetu;
b. Kufanya sensa za kitaifa na tafiti ili kukusanya takwimu muhimu kuhusu idadi ya watu na uchumi wetu; na
c. Kutoa taarifa za takwimu kwa serikali, sekta binafsi, na umma ili kusaidia sera na mipango.
Timu yetu yenye bidii na weledi inafanya kazi bila kuchoka chini ya kaulimbiu "Takwimu kwa Maendeleo" kuhakikisha Tanzania inapata takwimu inazohitajika katika kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu.
Kwa kuangalia mbele, NBS inajielekeza katika:-
a. Kutumia teknolojia na mbinu mpya ili kuboresha uwezo wetu wa ukusanyaji, uchakataji, uchambuzi na usambazaji wa takwimu;
b. Kuboresha upatikanaji na matumizi ya bidhaa zetu za takwimu;
c. Kuimarisha ushirikiano na wadau wa kitaifa na kimataifa;
d. Kuhakikisha viwango vya juu vya uadilifu wa takwimu na taaluma; na
e. Kukuza IMANI kwa wadau wote ndani na nje ya nchi.
Ninathibitisha tena kutekeleza Mkakati wa Mawasiliano, Ushawishi na Usambazaji wa Takwimu, ambao unalenga kuhakikisha tunakidhi mahitaji ya wadau wetu kwa kuzifanya bidhaa na huduma zetu zipatikane kwa urahisi na kwa namna rafiki kwa mtumiaji. Kuhakikisha kuwa tovuti yetu www.nbs.go.tz inaendelea kuwa chanzo cha kuaminika cha takwimu rasmi nchini.
Kwa hiyo, nina furaha kuwaalika kutembelea tovuti hii, ambayo ni mojawapo ya zana zinazopendelewa zaidi na wadau wetu kwa ajili ya usambazaji wa takwimu, na kutumia utajiri wa taarifa za takwimu tunazotoa. Ushirikiano wako na imani yako katika bidhaa na huduma zetu ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya taifa letu. Pamoja, tunaweza kutumia nguvu ya takwimu kuendeleza maendeleo na ustawi wa Tanzania.