Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Taifa ya Takwimu

Takwimu kwa Maendeleo
Kanuni za Msingi za Takwimu Rasmi

Kanuni ya 1: Takwimu rasmi ni hitaji la msingi katika mfumo wa taarifa katika jamii ya kidemokrasia, kuhudumia Serikali, uchumi, na umma kwa kutoa takwimu kuhusu hali ya kiuchumi, kidemografia, kijamii, na mazingira. Kwa madhumuni haya, takwimu rasmi zinazokidhi mahitaji ya matumizi halisi zinapaswa kukusanywa na kutolewa kwa uwazi na taasisi za kitakwimu ili kuheshimu haki ya raia ya kupata taarifa za umma.

Kanuni ya 2: Ili kuendeleza kuamini kwa takwimu rasmi, taasisi zinazozalisha takwimu zinahitaji kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia miongozo ya kitaalamu pekee, ikiwemo kanuni za kisayansi na kitaaluma ya takwimu.

Kanuni ya 3: Ili kuwezesha tafsiri sahihi ya takwimu, taasisi zinazozalisha takwimu zinapaswa kuwasilisha takwimu zake kwa kufuata viwango vya kisayansi kulingana na vyanzo, mbinu (methodolojia), na taratibu za kitakwimu.

Kanuni ya 4: Taasisi za kitakwimu zina haki ya kutoa ufafanuzi kuhusu tafsiri potofu na matumizi mabaya ya takwimu.

Kanuni ya 5: Taarifa kwa ajili ya madhumuni ya kitakwimu zinaweza kukusanywa kutoka kwenye vyanzo vya aina zote, iwe ni tafiti za kitakwimu au rekodi za kiutawala. Taasisi zinazozalisha takwimu zinapaswa kuchagua chanzo cha takwimu kulingana na ubora, upatikanaji kwa wakati, gharama, na kuepuka kumchosha mtoa taarifa/mhojiwa.

Kanuni ya 6: Taarifa ya mtu binafsi inayokusanywa na taasisi zinazozalisha takwimu kwa ajili ya uandaaji wa takwimu, ziwe zinahusiana na mtu binafsi au taasisi, zinatakiwa kutunzwa kwa usiri mkubwa na zitumike kwa madhumuni ya kitakwimu tu.

Kanuni ya 7: Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utendaji kazi wa mifumo ya kitakwimu zinapaswa kuwa wazi kwa umma.

Kanuni ya 8: Uratibu wa taasisi zinazozalisha kitakwimu ndani ya nchi ni muhimu ili kuepuka mgongano wa takwimu na kuleta ufanisi katika mfumo wa takwimu.

Kanuni ya 9: Dhana, uainishaji wa makundi ya kitakwimu, na mbinu za kimataifa zinazotumiwa na taasisi zinazozalisha kitakwimu katika kila nchi zinasaidia kukuza uepukaji wa mgongano wa takwimu, na kuleta ufanisi wa mifumo ya takwimu katika ngazi zote rasmi.

Kanuni ya 10: Ushirikiano na jumuiya za kimataifa katika masuala ya takwimu unachangia kuboresha mifumo ya takwimu rasmi katika nchi zote.