Dkt. Minja: Shindano la Ubunifu wa Kutumia Takwimu Fursa kwa Vijana
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Makazi na Takwimu za Kijamii, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS Dkt. Ruth Minja amesema Shindano la Ubunifu wa Takwimu kwa kutumia teknolojia ni fursa kwa vijana.
Dkt. Minja ameyasema hayo alipokuwa akizungumza wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC1, Dodoma mapema leo tarehe 24 Novemba 2025.
Amesema shindano hilo linalenga kuhamasisha vijana kutumia teknolojia kuandaa majibu ya ubunifu yatakayoboresha upatikanaji wa takwimu zilizopo mtandaoni ili ziweze kuwafikia Wananchi kwa uwazi na urahisi zaidi, pamoja na kutengeneza fursa mpya kwao.
Dkt. Minja amesema kupitia takwimu, vijana wataweza kuongeza ujuzi na kupata ajira kupitia maandiko na kazi watakazozalisha kulingana na mahitaji ya sekta mbalimbali kama afya, nishati na zinginezo.
Amebainisha kuwa washiriki wa shindano hilo wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, bila kujali jinsia, na muda wa mwisho wa kutuma maombi ni Desemba 10, 2025.
Washindi watapata zawadi ya fedha taslimu pamoja na mafunzo ya ziada ya takwimu, huku mshindi wa kwanza akipewa nafasi ya kufanya kazi na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.