The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Kikao Kazi cha Majumuisho ya Takwimu za Fedha za Serikali Mwaka 2024/2025
Posted On: 22 January, 2026
Kikao Kazi cha Majumuisho ya Takwimu za Fedha za Serikali Mwaka 2024/2025

Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS imeratibu na kushiriki katika kikao kazi cha majumuisho ya Takwimu za Fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za mwaka 2024/2025 kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ndogo ya NBS iliyopo Kivukoni jijini Dar es Salaam Januari 2026.

Kwa upande wake Mtakwimu Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Judith Jackson Uiso ambaye ndiye Mwenyekiti wa kikao hicho, amesema kikao hicho hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kujumuisha Takwimu za Fedha za Serikali kwa ngazi ya Serikali za Mitaa, Taasisi za Serikali, Mifuko ya Hifadhi za Taifa, Serikali Kuu na kusimamia taarifa za mapato, matumizi, uwekezaji wa Serikali na madeni kwa ngazi hizo za Serikali.

Uiso amesema lengo ni kupata hali ya mapato na matumizi ya Serikali na kutoa taarifa kwa wadau mbalimbali kwa kisekta, kimataifa na wadau wa ndani wanaotumia taarifa hizo ambazo huchapisha na kusambazwa kupitia vitabu vya bajeti, vikao Maalum na katika mifumo wa taarifa wa Shirika la Fedha la Kimataifa - IMF.

Kikao kazi hicho kimejumuisha Wachumi, Wahasibu na Watakwimu kutoka Wizara ya Fedha, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar - OCGS, Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OW – TAMISEMI), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii - NSSF, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma - PSSSF, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi - WCF na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya – NHIF.