NBS Launches Household Energy Consumption Survey 2023
Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS imezindua Ripoti ya Utafiti wa Matumizi ya Nishati katika Kaya ya mwaka 2023 katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Ngorongoro uliopo Ofisi za NBS Dodoma tarehe 17 Novemba 2025.
Ripoti hiyo ambayo imefadhiliwa na Umoja wa Ulaya - EU kupitia Shirika la Maendeleo la Expertise France, imezinduliwa rasmi na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadilifu Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga ambapo amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha Wananchi wanapata Takwimu sahihi na za kuaminika kuhusu namna wanavyotumia aina mbalimbali za nishati nyumbani mwao.
Mhandisi Luoga amezipongeza timu zote zilizoshiriki katika utafiti huo zikishirikisha Wataalamu wa Takwimu na Watafiti wa Nishati, kwa kazi nzuri ya kitaalamu iliyofanikisha kupatikana kwa ripoti hiyo muhimu kwa matumizi ya mipango ya Serikali na Wadau mbalimbali wa maendeleo.
Ameongeza kuwa Nishati ni muhimu katika uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji wa huduma zinazozingatia teknolojia rafiki kwa mazingira, Dira ya Maendeleo 2025/2050 na Malengo ya Maendelo Endelevu – SDG’s.
Kiongozi huyo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutumia matokeo ya utafiti huo kama nyenzo muhimu katika kupanga na kutekeleza sera bora za nishati zinazolenga kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata nishati ya uhakika, nafuu na endelevu.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema miongoni mwa madhumuni ya NBS siku zote ni kuboresha mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa takwimu bora kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo ya nchi na upimaji wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.
“Utafiti huu unatekeleza Lengo Namba Saba la Malengo ya Maendeleo Endelevu – SDG’s 17 ambalo linahitaji Wananchi wote kuwa wanatakiwa kupata nishati nafuu na ya kuaminika endelevu na safi ifikapo 2030.” Amesema Dkt. Msengwa na kuongeza;
“Ripoti hii ya mwaka 2023 inawasilisha kwa mara ya kwanza takwimu za matumizi ya nishati katika kaya kwa ujumla kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.”
Dkt. Msengwa amesema matokeo ya ripoti hiyo yanaonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na jitihada za Serikali pamoja na maeneo yanayohitaji kuimarishwa.
Amesema Takwimu zinaonesha kuwa kitaifa Asilimia 52 ya Kaya zinatumia umeme ambapo mjini ni Asilimia 72.7 na kijijini ni Asilimia 30.7 ambapo ameeleza kuwa hiyo ni dalili ya mafanikio ya Mradi ya Umeme Vijijini - REA na juhudi za Serikali kupanua Gridi ya Umeme ya Taifa.
Aidha, Dkt. Amina amesema kuhusu nishati ya kupikia matokeo yanaonesha kuwa Asilimia 66 ya Kaya hutumia kuni, Asilimia 44 hutumia mkaa, Asilimia 25 hutumia gesi na Asilimia 2 pekee hutumia umeme kwa kupikia ambapo amefafanua kuwa Takwimu hizo zinakumbusha umuhimu wa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya ya Wananchi na mazingira yake kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa matokeo hayo yatumike kama nyenzo ya kupanga sera, miradi na mipango ya maendeleo itakayochochea upatikanaji wa nishati safi, nafuu na endelevu kwa Watanzania wote.
Kiongozi huyo ametumia nafasi hiyo kuushukuru Umoja wa Ulaya na Shirika la Maendeleo la Expertise France kwa kutoa rasilimali fedha na utalaamu uliowezesha kufanya utafiti huu.
Akizungumza awali Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Expertise France, Lydia Mugarula ameishukuru Wizara ya Nishati na NBS kwa ushirikiano mkubwa ambao wameuonesha katika shughuli na miradi, ikiwemo uandaaji wa Ripoti hiyo ambayo imefanywa kwa ushirikiano wa taasisi zote zilizoko chini ya Wizara ya Nishati ikiwepo Wakala wa Umeme Vijijini – REA, Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania - TANESCO, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji - EWURA, Shirika la Maendeleo ya Petroli - TPDC, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli – PURA na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja - PBPA.
Ameongeza kuwa wataendelea kuwa jengea uwezo wa kutosha watumishi na waandaaji wa ripoti hizo ili kuifanya miradi hiyo iendelee kuwa endelevu.
Naye, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi - NBS, Daniel Masolwa amesema nishati ni kiashiria muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na jamii kwani kuna uhusiano wa karibu kati ya kiwango cha nishati na aina ya nishati inayotumika na kiwango cha maendeleo ya kiuchumi, ambapo amefafanua kuwa nchi zote zenye kiwango kikubwa cha nishati zina kiwango cha juu cha maendeleo ya kiuchumi na hali ya maisha ya Wananchi wake ipo juu.
Mkurugenzi huyo amesema kwa upande wa Tanzania pato la wastani ni dola 1,220 lakini kuni na mkaa unaotumika kwa kupikia katika kaya ni Asalimia 70 ilhali kwa Uganda wastani wa pato la Mwananchi ni dola 960 na nishati ya kuni na mkaa inayotumika kwa ajili ya kupikia ni asilimia 94 wakati Kenya pekee, pato la wastani ni dola 2,110 ambapo kuni na mkaa unaotumika kwa ajili ya kupikia ni Asilimia 49. Hivyo, amesema kadri kiwango cha uchumi kinapokwenda juu, ndivyo matumizi ya nishati za kuni na mkaa inavyozidi kupungua.
Akifunga hafla hiyo Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, amesema Utafiti huo unatoa taswira ya hali matumizi ya nishati nchini.
Mhe. Makinda amesema Ripoti hiyo inasaidia kuelewa changamoto, fursa na maeneo yanayohitaji kipaumbele ikiwemo kuandaa mikakati madhubuti ya kuongeza upatikanaji wa nishati safi hususan vijijini, kuwekeza katika teknolojia, miundombinu na program za kuhamasisha matumizi ya nishati salama, kupanga na kutenga rasilimali kulingana na mahitaji ya Wananchi, kufatilia kwa ufanisi utekelezaji wa malengo ya kitaifa na kimataifa pamoja na malengo ya sekta ya nishati.