The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
NBS Yawaita Vijana
Posted On: 25 November, 2025
NBS Yawaita Vijana

Meneja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Mwanaidi Mahiza, ametoa wito kwa vijana na wadau mbalimbali kushiriki katika shindano la ubunifu wa takwimu ambalo litaongeza mwamko na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kitakwimu kwa Wananchi.

Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Good Morning cha Wasafi FM mapema leo Jumanne tarehe 25 Novemba 2025, Mahiza amesema shindano hilo linatarajia kuibua bunifu mpya zitakazosaidia Wananchi kupata takwimu kwa urahisi, kwa wakati, na kwa njia bunifu zinazogusa maisha yao kila siku.

“Tunataka upatikanaji wa takwimu uwe rahisi zaidi kwa Mwananchi wa kawaida. Tunataka vijana waje na ubunifu utakao hakikisha takwimu tunazozalisha zinawafikia Wananchi kwa njia rahisi, hata mama anayefanya kazi sokoni aweze kuelewa kwamba takwimu zinatumika vipi.” Amesema Mahiza.

Mahiza, amesema kuwa shindano hilo litakuwa wazi kwa watanzania wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea.washiriki wanaweza kuunda vikundi vya watu wiwili hadi wa tano.

Amefafanua kuwa zawadi mbalimbali zinatarajiwa kutolewa kwa washindi ikiwepo nafasi wa kufanya kazi kwa mwaka mmoja katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu, vifaa vya TEHAMA Pamoja na fedha taslimu.

Naye, Meneja wa Sensa ya Watu na Takwimu za Matukio Muhimu ya Binadamu, Ofisi ya taifa ya Takwimu- NBS, Seif Kuchengo, amesema lengo la ubunifu katika takwimu si kukusanya taarifa na kuzihifadhi kwenye makabati, bali kuhakikisha zinasogezwa karibu na Wananchi kwa matumikzi ya kila siku.

"Takwimu hizi, kadiri zinavyotumika, sisi ndio tunapata faraja kwamba kazi yetu inaenda vizuri.” Amesema Kuchengo.

Shindano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa la kukuza ubunifu wa vijana, kuongeza matumizi ya Takwimu nchini na kuimarisha maamuzi ya maendeleo yanayotegemea taarifa sahihi.