The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
RC Mtanda Urges Statisticians to Provide Accurate Data to Drive Development
Posted On: 21 November, 2025
RC Mtanda Urges Statisticians to Provide Accurate Data to Drive Development

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda ametoa rai kwa Wataalamu wa Takwimu nchini kuchakata kwa weledi na kutoa Takwimu na Taarifa sahihi kwa jamii ili kuwapa mwelekeo wa shughuli za kufanya kwa wakati fulani ili kupata maendeleo.

Mhe. Mtanda ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na Wataalamu wa Takwimu wa Ofisiya Taifa ya Takwimu – NBS kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Mara, Kagera na Geita, waliokutana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba – TMDA, jijini Mwanza tarehe 18 Novemba, 2025.

RC Mtanda amesema Wananchi wanapanga maisha yao kiuchumi na kijamii kwa kutegemea taarifa sahihi kutoka serikalini mathalani kuhusu bei za bidhaa au hali ya upatikanaji wa pembejeo hivyo, wanawategemea kuwapatia taarifa sahihi za namna gani waenende.

“Mipango, taarifa na takwimu sahihi ndizo zinazotuwezesha kufanya makadirio ya maisha ya baadaye hivyo basi ninyi ndio wataalamu mnaotegemewa kufanya utafiti na kutumia ubunifu wa kuchakata na kutoa taarifa sahihi kwao ili kuwapa mwelekeo hivyo siku zote lazima muzingatie hilo.” Amesema RC Mtanda.

Aidha, ameongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025/2050 inawategemea Wataalamu hao kuweka misingi na mikakati ya uwekezaji na uwajibikaji katika kila sekta ambapo amesisitiza kuwa Takwimu zina faida kubwa kwenye kupanga mifumo ya maamuzi sahihi ya maendeleo.

Akimuwakilisha Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Daniel Masolwa ametoa rai kwa Wananchi kutoa ushirikiano kwa Watumishi wa NBS wanapofika kwa ajili kuchukua taarifa na takwimu kwa kuwa takwimu hizo zinatumika katika kupanga maendeleo.

Kwa upande wake Meneja wa Takwimu Msaidizi NBS Mkoa wa Mwanza, Abdallah Chengo amesema Takwimu zinasaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Kwa kuwa mchakato wa ukusanyaji wa taarifa unahitaji usahihi na usiri, kwa sababu hiyo, Wananchi hawapaswi kuwa na hofu, Wananchi wanatakiwa kuwa na ujasiri na kutoa ushirikiano…kwa hayo yote, tunahitaji kutumia teknolojia na ubunifu ili kuhakikisha kuwa matumizi ya takwimu yanasaidia kufanikisha maendeleo ya nchi.” Amesema Chengo.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika 2025 ambayo husherehekewa tarehe 18 Novemba kila mwaka inasema: “Kuongeza ubunifu katika matumizi ya takwimu na taarifa ili kujenga jamii jumuishi inayojali haki, amani na maendeleo ya Afrika.”