SG Dkt. Msengwa Azungumza, Kutoa Zawadi kwa Wanafunzi
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amezungumza na Wanafunzi wa Shule za Sekondari Dodoma na Wella, waliofika katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika tarehe 18 Novemba 2025 katika Ukumbi wa Ngorongoro uliopo Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Dkt. Msengwa amewaeleza Wanafunzi hao kuwa majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS ni kukusanya, kuchakata na kusambaza takwimu rasmi nchini, kushauri na kutoa vipaumbele kwa ajili ya Serikali kufanya mipango na kuratibu mfumo mzima wa takwimu ili kupanga na kuleta maendeleo kwa Wananchi ikiwemo huduma za kijamii.
Katika hatua nyingine Dkt. Msengwa ameendesha Shindano la Kitakwimu kwa kuwauliza maswali mbalimbali ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ambapo Wanafunzi waliojibu kwa usahihi, amewatunuku zawadi mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine, Kiongozi huyo amewahimiza Wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao ikiwemo kuja kuwa Watakwimu wazuri wa baadaye.
Naye, Mwakilishi wa Walimu walioongozana na Wanafunzi hao, Mwalimu Rosemary Msanya kutoka Shule ya Sekondari Wella, ameishukuru NBS kwa kuwapa nafasi ya kushiriki maadhimisho hayo na kuwa wamejifunza umuhimu wa Takwimu kwa Mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla katika kuleta maendeleo na kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha matumizi ya takwimu kwa jamii inayowazunguka.