The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics Tanzania

Statistics for Development
Takwimu ni Muhimu kwa Kila Mtu: Karugendo
Posted On: 20 October, 2025
Takwimu ni Muhimu kwa Kila Mtu: Karugendo

Mkurugenzi wa Uratibu waTafiti na Shughuli za Kitakwimu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS, Emilian Karugendo amesema takwimu ni muhimu kwa kila mtu katika maisha ya kila siku, kwa kuwa zinasaidia kufanya maamuzi sahihi katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Karugendo ameyasema hayo mapema leo tarehe 20 Oktoba 2025 alipokuwa akizungumza kwenye Kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC 1 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Takwimu Duniani ambayo huadhimishwa kila baada ya miaka mitano ambapo Kauli mbiu mwaka huu ni “Takwimu na Taarifa Bora kwa Kila Mtu.”

Karugendo amesema kuwa hata katika maisha ya kawaida ya nyumbani mtu anayeandaa chakula anahitaji kujua idadi ya watu, vivyo hivyo anapokwenda sokoni lazima ajue idadi ya vitu anavyohitaji na fedha atakazotumia kununua mahitaji yake.

“Takwimu anazihitaji kila mtu, na ni muhimu kwa kila mtu, si kwa ajili ya wasomi tu ni kwa ajili ya kila mtu, ni muhimu kwa maisha ya kila siku, kwa mtu wa kawaida, tuanzie kwenye familia…kabla mama au mtu yeyote hajaandaa chakula nyumbani hajaingia jikoni ni lazima ajue anaandaa nini kwa ajili ya nani.” Amesema Karugendo.

Ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ina jukumu la kuzalisha na kusambaza takwimu rasmi nchini kwa matumizi ya Serikali, Wadau wa Maendeleo na Wananchi kwa Ujumla ambapo pia ina jukumu la kuratibu uzalishaji wa takwimu nchini.   

Ameeleza kuwa Takwimu zinazosanywa kupitia vyanzo tofauti kama sensa na tafiti mbalimbali kama za kilimo, mifugo, afya na mazingira pamoja na taarifa za kiutawala zinatoa mwanga wa kuelewa tulipotoka, tulipo na tunakoelekea kama taifa katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050.

Karugendo amesisitiza kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu inatumia teknolojia katika ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa takwimu na taarifa sahihi ili kuongeza uwazi, ufanisi na uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya takwimu katika maisha ya kila siku kwa haraka.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa taasisi nyingine zinazoruhusiwa kuzalisha na kusambaza takwimu nchini, zinafanya hivyo chini ya Uratibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ili kuhakikisha uwiano na ubora wa taarifa zinazotolewa kwa umma.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo akizungumza kwenye kipindi cha Morning Trumpet cha UTV leo tarehe 20 Oktoba 2025, amesema kwa mwaka 2025 Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kutekeleza tafiti mbalimbali ikiwemo Utafiti wa Nguvu Kazi, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, uwezi wa Wananchi katika masuala ya kifedha, mapato na matumizi ambao huwa unatupatia taarifa na viwango vya umasikini kwa nchi.

Pia, Karugendo amesema kuwa NBS inafanya tafiti za kila mwezi ikiwemo utafiti wa mfumuko wa bei ambao taarifa yake hutolewa kila tarehe 08 ya kila mwezi.

Ameeleza kuwa utaratibu wa kufanya utafiti na kutoa takwimu rasmi ni kwamba taasisi au wadau wanaohitaji kufanya hivyo wanapaswa kuwasilisha maombi rasmi kwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali kueleza lengo la utafiti, njia zitakazotumika na gharama za utafiti ili kuhakikisha kuwa takwimu zitakazopatikana zinakidhi viwango vinavyotakiwa kitaifa na kimataifa.

Karugendo amesema takwimu zinazozalishwa hutumika katika kupanga sera, mipango na maamuzi ya maendeleo kwa taifa. Aidha, amewataka Wananchi na wadau mbalimbali kutumia takwimu hizo rasmi zinazopatikana kupitia Tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (www.nbs.go.tz), mitandao ya kijamii ya NBS na kupitia ujumbe mfupi wa simu za mkononi.