The United Republic of Tanzania

National Bureau of Statistics

Statistics for Development
Wadau Wahakiki Ripoti za Kina Tisa za Sensa ya Watu na Makazi ya 2022
Posted On: 13 November, 2025
Wadau Wahakiki Ripoti za Kina Tisa za Sensa ya Watu na Makazi ya 2022

Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar - OCGS imewasilisha kwa wadau Ripoti za Kina tisa zitokanazo na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 katika kikao cha uwasilishaji wa Ripoti hizo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro uliopo Makao Makuu ya Ofisi za NBS jijini Dodoma hivi karibuni.

Akifungua kikao hicho Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema Ofisi hizo zinaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa taarifa zinazokusanywa hazibaki ndani ya mikono ya NBS na OCGS bali ziwe chachu na muendelezo wa kuhakikisha kuwa zinaendelea kutumika katika kufanya tathmini bora kwa kuzingatia takwimu rasmi zinazozalishwa.

Akizungumza awali Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Makazi na Takwimu za Jamii, Dkt. Ruth Minja ameeleza kuwa, kufanyika kwa kikao hicho ni hatua muhimu ya maandalizi ya ripoti za kitakwimu katika kuhakikisha kuwa uchambuzi uliofanyika unakidhi vigezo vya ubora vya ndani na vya Umoja wa Mataifa (UN Fundamental Principles of Official Statistics). Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ripoti hizo zinaakisi hali halisi ya mahitaji ya takwimu kwa ajili ya kuwezesha kupanga, kupima na kutathmini hali ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya ndani, kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake Mtaalamu Mshauri, Dkt. Dadi Rutasha amesema sensa inaongoza kwa utajiri wa taarifa na kuwa ni chanzo kikubwa cha takwimu kwa ajili ya mipango na sera kwa mamlaka husika ambapo unaweza kupata taarifa hadi ngazi ya chini ya jamii. Hivyo, amehimiza matumizi ya taarifa hizo kwa Serikali na Wadau wa Maendeleo katika  kuandaa sera mbalimbali.

Ripoti zilizowasilishwa na kuhakikiwa na wadau ni zile za Hali ya Makazi na Rasilimali za Kaya, Vifo vya Utotoni, Vijana wa Rika Balehe na Ujana, Ajira na Shughuli za Kiuchumi pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Ripoti nyingine zilizowasilishwa ni Takwimu za Mtazamo wa Kijinsia, Uhamiaji na Ukuaji wa Miji, Vizazi na Vifo pamoja na Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.

Aidha, akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Salum Kassim Ali amewashukuru washiriki na wandaaji wa ripoti hizo ambapo amewahimiza kufanyia kazi na kukamilisha haraka maboresho yaliyotolewa na wadau ili ziweze kuzinduliwa na kusambazwa kwa ajili ya kutumika kwenye mipango, sera kwa maendeleo ya jamii.