Ripoti za Nishati
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Ofisi ya Takwimu Norway ilifanya tafiti za Athari ya Upatikanaji wa Nishati Endelevu kati ya mwaka 2019 na 2022. Tafiti hizi zilifanyika Tanzania Bara na zilifanyika kwa kutumia fedha za Serikali na za ufadhili wa Wakala wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Norway (Norad). Taarifa ya hivi karibuni inatoa viashiria vya kujibu lengo namba 7 (SDG 7.1) la Malengo Endelevu ya Dunia. Lengo namba 7 linabainisha mahitaji ya kuwa na nishati ya gharama nafuu, inayoaminika, endelevu na nishati ya kisasa ifikapo mwaka 2030. Tanzania Bara inatumia baadhi ya viashiria vya msingi kubainisha upatikanaji wa nishati. Tafsiri ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye kaya ni uwepo wa nguzo za kusambaza umeme katika Kijiji, kitongoji au mtaa. Kwa kuzingatia tafsiri hii, matokeo yanabainisha upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye kaya ni asilimia 72. Vilevile, kaya inakuwa imeunganishwa kwenye nishati ya umeme ikiwa ina balbu ya umeme angalau moja. Aidha, kwa mujibu wa matokeo hayo kaya zilizounganishwa kwenye nishati ya umeme iliongezeka kutoka asilimia 32.8 mwaka 2016/17 hadi asilimia 45.8 mwaka 2021/22, ikimaanisha kuwa zaidi ya kaya milioni 2 Tanzania Bara zilikuwa zimeunganishwa kwenye nishati ya umeme katika kipindi cha miaka sita.
Kwa taarifa zaidi wasiliana nasi kupitia anwani ya barua pepe: titus.mwisomba@nbs.go.tz